MKUU wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amesema kambi ya Matibu ya madaktari bingwa na bobezi ya kanda ya Kati imesogeza huduma za afya kwa wananchi ikiwa ni mpango wa Rais wa kutoa huduma bora na kwa urahisi.
Nyongo ameyasema hayo kwenye Hospitali ya Mkoa wa Pwani Tumbi wakati akizindua kambi ya matibabu bingwa na bobezi kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani kuanzia leo Novemba 16 hadi 20 mwaka huu.
Amesema kuwa kama inavyojulikana huduma za kibingwa na bobezi hupatikana kwenye baadhi ya hospitali na kwa nyakati maalum.
"Hapa tumesogezewa huduma kwa karibu na kwa urahisi hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili kuchunguza afya zao na kupatiwa matibabu ya kibingwa na bobezi,"amesema Nyongo.
Aidha amesema kuwa serikali imejenga vituo vingi vya afya nchini jambo ambalo ni muhimu kwa kupeleka huduma karibu kwa wananchi hivyo waitumie ili kujua afya zao.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Ukio Kusirye alisema kuwa tayari kambi ya madaktari bingwa na bobezi ya mabusha imefanyika Wilayani Kibaha ambapo imetolewa bure.
Kusirye amesema kuwa wanaendelea na utambuzi kwa ajili ya kambi ya macho kwenye Wilaya za Kisarawe na Mafia.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi Amani Malima amesema kuwa mwitikio wa watu kujitokeza ni mkubwa ambapo 600 wamejitokeza kwenye siku ya kwanza kati ya siku tano za kambi hiyo.
Malima amesema kuwa baadhi ya huduma zitatolewa bure ikiwa ni pamoja na kumuona daktari kisukari moyo ini mtoto wa jicho miwani na baadhi ya dawa.

No comments:
Post a Comment