MTAA wa Machinjioni Kata ya Tangini Wilayani Kibaha Mkoani Pwani umewataka mabalozi kuwatambua wageni wanaokwenda kuishi kwenye maeneo yao ili kudhibiti uhalifu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo Aidan Mchiwa alipokuwa akizingumza kwenye kikao cha wananchi na mabalozi juu ya kukabili vitendo vya uhalifu.
Mchiwa amesema kuwa baadhi ya wananchi wamelalamika kuongezeka vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya vijana ambao wamekuwa wakitumia visu kupora watu.
"Tuna ulinzi Shirikishi ambao tuna uhuisha ila wakati tunachukua hatu hizi mabalozi wahakikishe wanawatambua wageni wanaoingia kwenye maeneo yao kwa kuwasajili ili kupata taarifa zao,"amesema Mchiwa.
Amesema kuwa baadhi ya watu hasa vijana wamekuwa wakiingia kwenye maeneo ya Mtaa lakini taarifa zao hazipo hivyo ni rahisi kufanya uhalifu.
"Wageni wakifahamika pia kuwa na daftari la wakazi litasaidia kukabiliana na wahalifu kwani watu wote ndani ya Mtaa watakuwa wanafahamika itakuwa ni sehemu mojawapo ya mbinu za kudhibiti uhalifu,"amesema Mchiwa.
Aidha amesema kuwa wazazi wanapaswa kuwalea watoto wao kwenye maadili mazuri ili wasijiingize kwenye makundi ya uhalifu kwani endapo watabainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
"Pia baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwafumbia macho watoto wao ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uvutaji bhangi na kusababisha kushiriki kwenye uhalifu,"amesema Mchiwa.
Naye Mkazi wa Mtaa huo Gasper Assey amesema kuwa kuwa na daftari la wakazi ambapo kutakuwa na taarifa za wananchi wote itasaidia kupunguza uhalifu kwenye Mtaa huo.
Assey amesema kuwa hatua zichukuliwe kwa vijana ambao wanafahamika wanajihusisha na uhalifu na wazazi wasiwatetee watoto wao ambao ni wahalifu ndani ya Mtaa.

No comments:
Post a Comment