Monday, November 23, 2026

ELIACHAHOFU AELEZA MIPANGO YAKE KUWANIA UJUMBE BODI YA SIMBA SPORTS CLUB

MGOMBEA Ujumbe wa Bodi ya Simba Eliachahofu Paulo amesema kuwa endapo atachaguliwa kwenye nafasi hiyo atahakikisha analipa kipaumbele suala la usajili wa wanachama ili kuongeza mapato ya klabu.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Paulo amesema kuwa klabu ya Simba ina wanachama wengi ambao wanahitaji kusajiliwa ili kuichangia timu yao.

Paulo amesema usajili wa wanachama hauko vizuri na endapo utasimamiwa vizuri utaongeza mapato kupitia ada na michango mbalimbali itakayotakiwa kuichangia timu.

"Simba ni timu kubwa hivyo mtaji wake mkubwa ni kuwa na wanachama ambao watakapolipia viingilia na ada ya uanachama itafanya klabu kuwa na mapato makubwa,"amesema Paulo.

Amesema kuwa chanzo hicho ni muhimu lakini hakijapewa uzito hivyo kwake hicho kitakuwa ni kipaumbele katika kuhakikisha klabu inakuwa na mapato ya uhakika.

"Kingine ni kuweka ukaribu kati ya wanachama na viongozi wao ambapo viongozi wanapaswa kushuka kwenye matawi na kuwa karibu na wanachama ili kujadili maendeleo ya timu,"amesema Paulo.

Aidha amesema kama atachaguliwa kuwa mjumbe wa bodi ya Simba atapendekeza jinsi gani ya kupata wachezaji vijana wazawa badala ya kutegemea kutoka nje pia timu ya wanawake isaji wachezaji wa ndani wenye ubora badala kutegemea wa nje.

"Pia ni kuwekeza nguvu kubwa ili kuhakikisha tunakuwa na uwanja wetu badala ya kutegemea viwanja vya wenzetu kwani tumekuwa tukihangaika michezo yetu kuchezwa kwenye viwanja tofautitofauti hiyo yote inatokana na kutokuwa na uwanja wetu,"amesema Paulo.

Aliongeza kuwa anaipongeza timu yake ya Simba kufanya vizuri kwenye michezo yake ya Ligi Kuu na ni mategemeo yake itafanya vizuri na kutwaa kombe la ligi kuu na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment