WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Mwigulu Lamek Nchemba amesema kuwa upatikanaji wa vitambulisho vilivyoboreshwa ni kukuza shughuli za uchumi na upatikanaji wa huduma mbalimbali.
Nchemba ameyasema hayo Kibaha wakati akizindua Kitambulisho cha Taifa cha Nida kilichoboreshwa akimwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa mradi huo ni uwekezaji mkubwa na wa kisasa utakaotoa vitambulisho ambavyo vitakuwa na huduma nyingi kwa kuunganishwa na taasisi nyingine.
"Vitambulisho hivi vitapunguza usumbufu kuwa vitambulisho vingi vya taasisi nyingine na kuongeza ufanisi na uwekezaji huu utaleta matokeo ya Mtanzania apate kitambulisho kwa wakati na hili ni suala muhimu na la msingi,"amesema Nchemba
Aidha amesema kuwa kitambulisho kitasaidia kupata huduma na shughuli za kijamii kiuchumi na kitarahisisha masuala ya maendeleo.
"Kupitia mradi huu wa vitambulisho ni kutambuana na ni udugu pia nyenzo muhimu ya kuunganisha na kutambulisha kutambuana na katika kupata huduma za kijamii na ni utekelezaji wa dira ya maendeleo ya 2050 ya kuwa na matumizi ya teknolojia,"amesema Nchemba.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani Patrobas Katambi amesema kuwa hadi Oktoba mwaka mwaka huu vitambulisho vilivyozalishwa ni milioni 21.5 ambavyo wanavyo wananchi ni milioni 19.6 na ambavyo havijachukuliwa ni zaidi ya milioni moja.
Katambi amesema kuwa kiasi cha shilingi bilioni 30 zilitolewa kwa ajili ya mashine pamoja na kadi hivyo serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa vitambulisho.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA James Kaji amesema kuwa watu wote ambao vitambulisho vyao vimetoka hawajavichukua na wanatumia namba tu ni milioni 1.2 wamepewa miezi mitatu na endapo hawatavichukua vitafutwa.
Kaji amesema kuwa wamepewa magari 140 tofauti na mwanzo ambapo walikuwa na magari 28 hivyo bajeti imeongezeka mara tatu na kwa sasa kila Wilaya itakuwa na gari lake hadi kwenye visiwa vikiwemo vilivyopo ziwa Victoria vimepewa boti ili viweze kufikiwa kirahisi.
Alisema kuwa huduma zitakazounganishwa ni pamoja na cheti cha kuzaliwa bima ya afya namba ya utambulisho wa mfanyabiashara TIN grupu la damu hati ya kusafiria na utambulisho wa ndoa.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Ally Gugu amesema kuwa mradi huo wa vitambulisho vya taifa vilivyoboreshwa ni kusajili na kutambua na kuwapatia vitambulisho kuboresha utambuzi uchakataji na uzalishaji vitambulisho.
Gugu amesema kuwa dhamira ya serikali ni kutekeleza maendeleo ya taifa katika uwekezaji kuboresha mifumo undiklishaji salama na kwa wakati kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amesema kuwa wananchi watasaidiwa kupata vitambulisho bila ya foleni kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Nyongo amesema kuwa utambuzi wa wananchi kupitia vitambulisho vya utaifa ni kusimamia nguzo ya maendeleo na shughuli kufanyika kwa ufanisi na kiusalama itasaidia na utambulisho wa Mtanzania.

No comments:
Post a Comment