Wednesday, November 18, 2026

WAZIRI MKUU DK NCHEMBA ASEMA KITAMBULISHO CHA TAIFA KILICHOBORESHWA KUUNGANISHA HUDUMA MBALIMBALI

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Mwigulu Lamek Nchemba amesema kuwa upatikanaji wa vitambulisho vilivyoboreshwa ni kukuza shughuli za uchumi na upatikanaji wa huduma mbalimbali.

Nchemba ameyasema hayo Kibaha wakati akizindua Kitambulisho cha Taifa cha Nida kilichoboreshwa akimwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa mradi huo ni uwekezaji mkubwa na wa kisasa utakaotoa vitambulisho ambavyo vitakuwa na huduma nyingi kwa kuunganishwa na taasisi nyingine.

"Vitambulisho hivi vitapunguza usumbufu kuwa vitambulisho vingi vya taasisi nyingine na kuongeza ufanisi na uwekezaji huu utaleta matokeo ya Mtanzania apate kitambulisho kwa wakati na hili ni suala muhimu na la msingi,"amesema Nchemba

Aidha amesema kuwa kitambulisho kitasaidia kupata huduma na shughuli za kijamii kiuchumi na kitarahisisha masuala ya maendeleo.

"Kupitia mradi huu wa vitambulisho ni kutambuana na ni udugu pia nyenzo muhimu ya kuunganisha na kutambulisha kutambuana na katika kupata huduma za kijamii na ni utekelezaji wa dira ya maendeleo ya 2050 ya kuwa na matumizi ya teknolojia,"amesema Nchemba.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani Patrobas Katambi amesema kuwa hadi Oktoba mwaka mwaka huu vitambulisho vilivyozalishwa ni milioni 21.5 ambavyo wanavyo wananchi ni milioni 19.6 na ambavyo havijachukuliwa ni zaidi ya milioni moja.

Katambi amesema kuwa kiasi cha shilingi bilioni 30 zilitolewa kwa ajili ya mashine pamoja na kadi hivyo serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa vitambulisho.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA James Kaji amesema kuwa watu wote ambao vitambulisho vyao vimetoka hawajavichukua na wanatumia namba tu ni milioni 1.2 wamepewa miezi mitatu na endapo hawatavichukua vitafutwa.

Kaji amesema kuwa wamepewa magari 140 tofauti na mwanzo ambapo walikuwa na magari 28 hivyo bajeti imeongezeka mara tatu na kwa sasa kila Wilaya itakuwa na gari lake hadi kwenye visiwa vikiwemo vilivyopo ziwa Victoria vimepewa boti ili viweze kufikiwa kirahisi.

Alisema kuwa huduma zitakazounganishwa ni pamoja na cheti cha kuzaliwa bima ya afya namba ya utambulisho wa mfanyabiashara TIN grupu la damu hati ya kusafiria na utambulisho wa ndoa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Ally Gugu amesema kuwa mradi huo wa vitambulisho vya taifa vilivyoboreshwa ni kusajili na kutambua na kuwapatia vitambulisho kuboresha utambuzi uchakataji na uzalishaji vitambulisho.

Gugu amesema kuwa dhamira ya serikali ni kutekeleza maendeleo ya taifa katika uwekezaji kuboresha mifumo undiklishaji salama na kwa wakati kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amesema kuwa wananchi watasaidiwa kupata vitambulisho bila ya foleni kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Nyongo amesema kuwa utambuzi wa wananchi kupitia vitambulisho vya utaifa ni kusimamia nguzo ya maendeleo na shughuli kufanyika kwa ufanisi na kiusalama itasaidia na utambulisho wa Mtanzania.

KAGARUKI ATAKA WAHITIMU KIDATO CHA NNE KUZINGATIA MAADILI YA KITANZANIA

WANAFUNZI waliomaliza kidato cha nne Wilayani Kibaha wametakiwa watumie vizuri mitandao ya kijamii isiwaharibie ndoto zao za baadaye na kulinda maadili ya Kitanzania.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Katibu wa Siasa Uenezi na Mafunzo Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini Clemence Kagaruki ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 19 ya kidato cha nne Shule ya Sekondari Nyumbu.

Kagaruki amesema kuwa baadhi ya wanafunzi wahitimu wamekuwa wakijiingiza kwenye vitendo vya kinyume na maadili ya Kitanzania na kujikuta wakijiharibia taswira yao ndani ya jamii.

"Utandawazi siyo jambo baya kwani hatuwezi kuwa nyuma lakini wanafunzi wahitimu wa sekondari au wanavyuo wanapaswa kuitumia vizuri huku wakilinda maadili yetu ambayo ni mazuri tofauti na yale ya nchi zingine hasa zilizoendelea,"amesema Kagaruki.

Alisema wazazi wanapaswa kuwalinda watoto wao kwani mmomonyoko wa maadili ni mkubwa sana na unaweza ukasababisha kuwaharibia maisha yao ya baadaye na kupoteza ndoto zao.

"Kuhusu changamoto naahidi kuchangia kiasi cha shilingi 600,000 ziweze kusaidia kuzipunguza na tutaongea na wadau wa elimu ili wakabili chsngamoto hizi ili wanafunzi waweze kusoma kwenye mazingira mazuri,"amesema Kagaruki. 

Katika hatua nyingine aliwasiliana na Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo kwa njia ya simu ambaye aliahidi kuitembelea shule hiyo siku ya Alhamis ili akaangalie namna ya kukabili changamoto ya maji ambapo wanahitaji kuchimbiwa kisima.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Juma Mrope amesema kuwa licha ya shule kupata ufaulu mzuri lakini changamoto kubwa ni maji ambapo kila mwezi hutumia kiasi cha shilingi 400,000 ikiwa ni ankara ya maji.

Mrope amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa ukumbi wa mikutano maktaba viti meza samani ofisi ya walimu ukarabati vyumba vya walimu na ujenzi wa madarasa.

Jumla ya wanafunzi 300 walitunukiwa vyeti vya kuhitimu kidato cha nne ambapo shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,630.

Tuesday, November 17, 2026

WAZIRI MKUU DK MWIGULU NCHEMBA KUMWAKILISHA RAIS DK SAMIA SULUHU HASSAN UZINDUZI KITAMBULISHO CHA TAIFA KILICHOBORESHWA

WAZIRI Mkuu  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Mwigulu Nchemba anatarajiwa kumwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwenye uzinduzi wa kitambulisho cha taifa kilichoboreshwa

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha ambapo uzinduzi huo utafanyika Stendi ya zamani ya Maili Moja Manispaa ya Kibaha.

Nyongo amesema kuwa uzinduzi huo ambao una umuhimu mkubwa katika kuendeleza mfumo wa utambulisho wa wananchi na kuboresha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma nchini na umuhimu wa watu kuelewa kuwa uzinduzi huo si tukio la kutambulisha kitambulisho kipya pekee bali ni hatua muhimu katika kuboresha mfumo wa utambulisho wa Taifa. 

"Mbali ya uzinduzi wa Kitambulisho cha Taifa Kilichoboreshwa toleo la 2026 NIDA pia atazindua rasmi huduma mpya inayojulikana kama "HUDUMA BILA FOLENI", inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kupunguza muda wa wananchi kusubiri na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Mamlaka hiyo,"amesema Nyongo.

Amesema huduma zitakazotolewa zitahusisha usajili wa wananchi ambao bado hawajajisajili katika mfumo wa NIDA uhakiki na marekebisho ya taarifa za utambulisho pale inapobidi ufuatiliaji wa hatua na hali ya maombi ya Vitambulisho vya Taifa.

"Utoaji wa Vitambulisho vya Taifa vilivyokamilika kwa wananchi wenye namba ya utambulisho wa Taifa (NIN) ambao bado hawajavichukua kutoa elimu na ushauri kuhusu taratibu na huduma mbalimbali zinazotolewa na NIDA.

Aidha amesema kuwa uzinduzi huo unatoa fursa ya kipekee kwa wananchi kupata taarifa kutatua changamoto zinazohusu utambulisho wao na kunufaika na huduma za NIDA bila kulazimika kusubiri fursa nyingine.

"Natoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Pwani
kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo na kutumia fursa ya kupata huduma mbalimbali zitakazotolewa na NIDA na kumsikiliza Waziri Mkuu,"amesema Nyongo.

Katika hatua nyingine amesema Novemba 21 Waziri Mkuu atafanya ziara katika Halmashauri ya Chalinze ambapo atafanya Mkutano wa hadhara katika viwanja wa Polisi Chalinze.

Monday, November 16, 2026

SERIKALI YASOGEZA HUDUMA ZA AFYA ZA KIBINGWA NA BOBEZI KWA WANANCHI PWANI

MKUU wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amesema kambi ya Matibu ya madaktari bingwa na bobezi ya kanda ya Kati imesogeza huduma za afya kwa wananchi ikiwa ni mpango wa Rais wa kutoa huduma bora na kwa urahisi.

Nyongo ameyasema hayo kwenye Hospitali ya Mkoa wa Pwani Tumbi wakati akizindua kambi ya matibabu bingwa na bobezi kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani kuanzia leo Novemba 16 hadi 20 mwaka huu.

Amesema kuwa kama inavyojulikana huduma za kibingwa na bobezi hupatikana kwenye baadhi ya hospitali na kwa nyakati maalum.

"Hapa tumesogezewa huduma kwa karibu na kwa urahisi hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili kuchunguza afya zao na kupatiwa matibabu ya kibingwa na bobezi,"amesema Nyongo.

Aidha amesema kuwa serikali imejenga vituo vingi vya afya nchini jambo ambalo ni muhimu kwa kupeleka huduma karibu kwa wananchi hivyo waitumie ili kujua afya zao.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Ukio Kusirye alisema kuwa tayari kambi ya madaktari bingwa na bobezi ya mabusha imefanyika Wilayani Kibaha ambapo imetolewa bure.

Kusirye amesema kuwa wanaendelea na utambuzi kwa ajili ya kambi ya macho kwenye Wilaya za Kisarawe na Mafia.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi Amani Malima amesema kuwa mwitikio wa watu kujitokeza ni mkubwa ambapo 600 wamejitokeza kwenye siku ya kwanza kati ya siku tano za kambi hiyo.

Malima amesema kuwa baadhi ya huduma zitatolewa bure ikiwa ni pamoja na kumuona daktari kisukari moyo ini mtoto wa jicho miwani na baadhi ya dawa.

Friday, November 13, 2026

HALMASHAURI YA MANISPAA KIBAHA YAMUONDOA MZABUNI WA USAFI

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imeazimia kuiuondoa kampuni ya usafi ya Sosamy kwenye Halmashauri hiyo baada ya kushindwa kutoa huduma kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo kwenye kikao cha robo cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo.

Mawazo amesema kuwa kutokana na kushindwa huko menejimenti iweke utaratibu ili kupata kampuni nyingine ya usafi.

"Kamati zote za Baraza la Madiwani la Halmashauri zilikubaliana mzabuni asiendelee na kazi kutokana na kushindwa hivyo aondolewe,"amesema Mawazo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Fadhil Nkurlu ambaye alijitambulisha kwenye baraza hilo baada ya kuhamishiwa kwenye Wilaya hiyo akitokea Wilaya ya Songwe amesema kuwa kikubwa anachokitaka ni ushirikiano.

Nkurlu amesema kuwa angependa kila kiongozi atekeleze majukumu yake kwa kuzingatia taratibu zilizopo bila ya kuwa na tofauti ili utendaji kazi wa kuwatumikia wananchi uende sawa.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwajuma Nyamka amesema kuwa Madiwani hao wanapaswa kuwa wazalendo kwa kupambania maslahi ya wananchi.

Nyamka amesema kuwa wananchi wanataka tabasamu kwa kutatuliwa changamoto zao ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM ambapo ni maono ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Thursday, November 12, 2026

MABALOZI MTAA WA MACHINJIONI WATAKIWA KUTAMBUA WAGENI ILI KUDHIBITI UHALIFU.

MTAA wa Machinjioni Kata ya Tangini Wilayani Kibaha Mkoani Pwani umewataka mabalozi kuwatambua wageni wanaokwenda kuishi kwenye maeneo yao ili kudhibiti uhalifu.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo Aidan Mchiwa alipokuwa akizingumza kwenye kikao cha wananchi na mabalozi juu ya kukabili vitendo vya uhalifu.

Mchiwa amesema kuwa baadhi ya wananchi wamelalamika kuongezeka vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya vijana ambao wamekuwa wakitumia visu kupora watu.

"Tuna ulinzi Shirikishi ambao tuna uhuisha ila wakati tunachukua hatu hizi mabalozi wahakikishe wanawatambua wageni wanaoingia kwenye maeneo yao kwa kuwasajili ili kupata taarifa zao,"amesema Mchiwa.

Amesema kuwa baadhi ya watu hasa vijana wamekuwa wakiingia kwenye maeneo ya Mtaa lakini taarifa zao hazipo hivyo ni rahisi kufanya uhalifu.

"Wageni wakifahamika pia kuwa na daftari la wakazi litasaidia kukabiliana na wahalifu kwani watu wote ndani ya Mtaa watakuwa wanafahamika itakuwa ni sehemu mojawapo ya mbinu za kudhibiti uhalifu,"amesema Mchiwa.

Aidha amesema kuwa wazazi wanapaswa kuwalea watoto wao kwenye maadili mazuri ili wasijiingize kwenye makundi ya uhalifu kwani endapo watabainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

"Pia baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwafumbia macho watoto wao ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uvutaji bhangi na kusababisha kushiriki kwenye uhalifu,"amesema Mchiwa.

Naye Mkazi wa Mtaa huo Gasper Assey amesema kuwa kuwa na daftari la wakazi ambapo kutakuwa na taarifa za wananchi wote itasaidia kupunguza uhalifu kwenye Mtaa huo.

Assey amesema kuwa  hatua zichukuliwe kwa vijana ambao wanafahamika wanajihusisha na uhalifu na wazazi wasiwatetee watoto wao ambao ni wahalifu ndani ya Mtaa.


REMNANT YAICHAPA KIBAHA MC 2-0

REMNANT FC ya Machinjioni imeifunga timu ya Manispaa ya Kibaha bao 2-0 kwenye mashindano  ya Machinjioni Super Cup Season 1.

Mashindano hayo yanafanyika kwenye uwanja wa Bwawani Maili Moja Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.