Sunday, March 31, 2024

BONANZA LA WIZARA YA FEDHA BARA NA VISIWANI LAFANA





Na Wellu Mtaki, Dodoma

Bonanza la mpira wa miguu, kuvuta kamba na mpira mikono limefanyika leo Jijini Dodoma likiwashirikisha watumishi mbalimbali wa Wizara ya Fedha kutoka Bara na Visiwani.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala rasilimali watu Wizara ya Fedha Lusius Mwenda amesema kuwa lengo la bonanza hilo ni kudumisha ushirikiano na undugu kati yao.

Na kusema kuwa kuna tija inayopatikana ikiwemo kuimarisha urafiki wa pande zote mbili, kufahamiana na kuimarisha afya za Watumishi.

"Lengo kubwa katika mashindano ni Ushirikiano kati yetu,sisi huku Tanzania  Bara na wenzetu wa Zanzibar".

"Tija kubwa ambayo inapatikana ni pamoja na watumishi kuimarisha afya, kufahamiana  na kuwa na urafiki wa pande zote mbili, kwa mfano kwa sisi kwenda kule Zanzibar na wao kuja huku kama ambavyo tumekuwa tukifanya".

Akizungumza Mwakilishi kutoka Zanzibar Bwana Rajab Uweje ofisa Uendeshaji Ofisi ya Raisi fedha na mipango Zanzibar amesema kuwa  Tamasha hilo ni ishara nzuri tumelikuta na hivyo tuliendeleze.

"Kwanza bonanza hili tunajenga uhusiano baina yetu nichukue nafasi hii kuzishukuru Taasisi zetu mbili kutudhamini katika Tamasha hili na hiki ni kitu chema sana tumekikuta na hivyo kwahiyo tukiendeleze kwa vizazi vyetu".

Mwenyekiti wa Hazina Sports Club Mugusi Musita amezungumzia suala la mikakati ya uboreshaji wa Tamasha hili kwa muda mrefu ikiwemo kuongeza wigo wa timu shiriki katika Tamasha hili ambapo kwa mwaka huu wamefaniki na kuweza kuongeza timu mpaka kufika sita.

"Kawaida huwa tunacheza Hazina ya Tanzania Bara na Zanzibar lakini mwaka huu tumekuwa na timu sita kwa hiyo mikakati tuliyoiweka ni kuboresha kama kuongeza timu umeona kama polisi walikuwepo hapa lakini kujenga mahusiano mazuri na wenzetu sisi kama Wizara za Kimuungano wenzetu wa visiwani tunafanya kazi moja na ndo tunaboresha mahusiano na kuboresha afya".

Tamasha hili la Pasaka limekuwa likifanyika kwa zaidi ya miaka ishirini mpaka sasa.

Saturday, March 30, 2024

VIONGOZI WAASWA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI WAO - RAS MMUYA.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Kaspar Mmuya ameendelea na ziara yake ya kikazi ya ukaguzi wa miradi na kuongea na watumishi kwa lengo la kujitambulisha Katika Halmashauri za Mkoa wa Dodoma ambapo Leo Machi 28, 2024 ametembelea Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma Mjini.

Kufuatia uzinduzi wa kampeni ya "Kero yako wajibu wangu", Mmuya ameendelea kuwa sisitiza watumishi kuwa na wajibu wa kusikilza na kutatua kero za wananchi kwa nafasi zao. Hayo ameyasema katika Kikao chake na watumishi wa Halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Umonga Jijini Dodoma.

“Ni vyema kujua vipaumbele na  wajibu wako wa Kusikiliza Kero za wananchi wanaotuzunguka tukiwa wawakilishi wao na uongozi mliopewa una jukumu la kutatua kero za wananchi katika Mitaa yetu na dhana ya kuwajibika inaenda Sabamba na utaratibu na kuipa ubora kazi yako.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anawajibika ipasavyo kwa kuleta fedha za miradi katika jamii na kama Msimamizi wa hizo fedha unapaswa kuzingatia ubora wa majengo yanayojengwa na kama kiongozi wajibu wako ni kuhakikisha hizo fedha zinatumika vizuri kama ilivyoelekezwa na usiwe chanzo cha kuwa kero kwa wengine," Amesema. Mmuya.

Vilevile, ametilia mkazo suala la kuongeza ufaulu mashuleni, kuondoa utoro kwa wanafunzi, upandaji na utunzaji miti, mahusiano bora mahala pa kazi, uwajibikaji katika kila ngazi aliyonayo mtu.

Aidha, Katibu Tawala Mkoa amekagua mradi wa ujenzi wa Madarasa 08 na matundu 10 ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi wa Kidato cha tano katika shule ya Sekondari Mtumba iliyopo kwenye kata ya Mtumba ambayo ilipokea fedha kiasi cha shilingi Milioni 201.

Mradi mwingine ni ujenzi wa vyumba 08 vya madarasa na matundu 10 ya choo katika shule ya Sekondari Zulu iliyopokea kiasi cha shilingi Milioni 201 na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya iliyopokea shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Maabara, jengo la wagonjwa wa nje ( OPD), jengo la mama na mtoto, Jengo la Mionzi, Jengo la Dawa, jengo la kuhifadhia maiti na kichomea taka.

Friday, March 29, 2024

*DKT.SHEMWELEKWA AWAFUNDA WATUMISHI KIBAHA.*

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa siku ya Jumatano 27 Machi,2024 amefanya kikao rasmi na watumishi kwa lengo la kufahamiana, kujitambulisha na kutoa mwelekeo kiutendaji.

Dkt.Shemwelekwa aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan tarehe 13 Machi,2024 kuwa Mkurugenzi wa Kibaha Mji amesifu mifumo mizuri iliyowekwa na Watangulizi wake akiwemo Bi.Jenifa Omolo ambaye kwa Sasa ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mhandisi Mshamu Munde aliyehamishiwa Halmashauri ya Nanyamba na kwamba kazi yake Sasa ni kutengeneza kemia mpya itakayotumika ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi 

Dkt.Shemwelekwa amewataka watumishi kutoa huduma Bora kwa wananchi wakiwa na furaha,kuondoa hofu,woga na wasiwasi na kwamba unapokuwa ofisini mwananchi ana matumaini makubwa nawe ya Kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zake.

Aidha,Dkt.Shemwelekwa amewaasa watumishi kuwa wanyenyekevu kwa wananchi,kutumia lugha za staha,kuheshimiana,kushirikiana,kupendana na kusaidiana ili kufanya kazi zenye matokeo na zinazoacha alama za kukumbukwa huku akikemea vikali tabia za kufanyakazi kwa mazoea zisizokuwa na tija kwa Taifa letu.

"Watumishi wa Umma tuache kulalamika,tujielekeze kwenye kuondoa malalamiko na kero za wananchi.Tuwasikilize vizuri na kuwahudumia tukiwa na furaha"...amesema Dkt.Shemwelekwa.

Akizungumzia ukusanyaji wa Mapato ametoa rai kwa watumishi wote kushiriki na sio kuwaachi Kitengo cha fedha na Divisheni ya Biashara pekee kama ilivyozoeleka huku akitoa rai ya kuongeza uadilifu,uaminifu na kuziba mianya yote inayovujisha ama kuchepusha Mapato na kwamba atakayefanya hivyo hata mvumilia.

"Ndugu zangu tukakusanye Mapato kwa uaminifu na uadilifu ili yatumike kwa Maslahi mapana ya watu wote,atakaye thubutu kwenda kinyume atakumbana na mkono wa sheria" ameongeza

Dkt.Shemwelekwa amekumbusha watumishi kuwahi Kazini kama sheria,Kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma zinavyoelekeza na kwamba hiyo sio hiari ni takwa la Kisheria linalomtaka mtumishi kufanya kazi kwa saa nane kwa siku

Mary Chimoto na Hassan Ngonyani  wamesifu utaratibu mpya kiutendaji wa Mkurugenzi Dkt.Shemwelekwa na kwamba kilichobaki ni utekelezaji 

Mkuu wa Divisheni na Utumishi na rasilimali watu Dibogo Protas amesema kazi yake kwenda kutafsiri sheria,Kanuni na taratibu kwani watumishi Sasa wamekumbushwa upya wajibu wao.


Dkt.Rogers Shemwelekwa ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutumiza miaka mitatu Madarakani kwa kuendelea kuwekeza kwenye Miradi mikubwa ya Kimkakati nchini ikiwemo Kibaha Mji ambayo imenufaika na Soko kubwa lenye thamani ya Bilioni nane

MWENYEKITI UVCCM WILAYA YA MPWAPWA AFURAHISHWA NA SOKA



Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana UVCCM Wilaya ya Mpwapwa Yohana Malogo ameendelea na ziara yake katika Kata ya Godegode kimagai na vingh'awe katika kijiji cha isingh'u

Akiwa katika kata ya Vingh'awe kijiji cha Ising'u ameshudia mechi Kati ya Miondo Fc dhidi ya Bondeni Fc

Ambapo amesema Mpira ni Mchakato na mwezi wa tano watakuwa na ligi ya Ngo'mbe

"Tumeona tufike hapa tuone mchezo wenu lakini pia tuwasalimie na tufahamiane"Amesema Malogo

"Tuwaombe tushirikiane,karibuni Ofisini kwetu ile Ofisi siyo ya kwangu,wala siyo ya katibu ni Ofisi yenu vijana Wilaya nzima yakuwasilisha changamoto na matatizo na adha zote zinazohusu vijana kwenye idara ya michezo na idara zingine"Amesema

Naye Katibu wa Umoja wa Vijana UVCCM Wilaya hiyo Alhabib Kibamba amesema kuwa kwa sababu ya serikali imesimama vizuri chini ya Chama Cha Mapinduzi ndo maana tuna amani na tunacheza tukiwa na furaha

Kwa Upande wake Diwani wa kata hiyo ya Vingh'awe Mahuwi Dickson amesema kuwa lengo la bonanza ni kuwaweka vijana pamoja,na Kujenga Mahusiano mazuri baina ya vijana

"Mashindano haya ni ya kata ni vijana ambao wanatoka katika eneo langu la kata mwisho wa siku nahitaji vijana hawa nipate timu bora ambayo sasa nitashirikisha na kata ya jirani"amesema

Aidha ameongeza kuwa mei mosi wataanza tena mashindano ya kushindania Ngo'ombe.

Wednesday, March 27, 2024

BMH YAITEMBELEA WIZARA YA AFYA NA HOSPITALI YA LUMUMBA ZANZIBAR

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma inatarajia kuanzisha ushirikiano wa matibabu na Hospitali ya Rufaa ya Mjini Magharibi (Lumumba), Zanzibar katika huduma za kibingwa. 

Ushirikiano huu utalenga kubadilishana uzoefu kati ya Hospitali hizi mbili za umma.

Akiongea, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe.Hassan Khamis Hafidh, amepongeza ujio wa Viongozi wa BMH na kuwa Hospitali ya Lumumba itanufaika kwa kubadilishana uzoefu.

"Nimefika Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma nikajionea utayari wa Madaktari Bingwa na Vifaa vya kisasa mnavyovitumia, nimefika kwenye wodi maalumu ya Uloto nikiri kwamba naona fahari kuja kwenu hapa maana yapo mengi tutakayo chukua kupitia ushirikiano huu," amesema Mhe Naibu Waziri.

Ameyasema hayo wakati uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa ulipomtembelea ofisini kwake.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bi. Prisca Lwangili, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, amesema "Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa kwa kasi na kutoa matibabu ambayo hayapatikani Afrika Mashariki na Kati.

"Hivyo tumeona ni muhimu kusogeza huduma hizi hapa Zanzibar kwa kuwa hapa pia kuna uhitaji wa huduma za Upandikizaji Uloto ili kutibu seli mundu," amesema. 

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo wa BMH, Bi. Monica Kessy, uhusiano huu ni sehemu ya wajibu wa BMH ili kubadilishana uzoefu kati ya hospitali za umma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji BMH, Dkt. Januarius Hinju, ameeleza utayari kwa Madaktari Bingwa wa BMH katika huduma.

"Madaktari Bingwa wa BMH tupo tayari kushirikiana na wenzetu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora," ameongeza.

WANAFUNZI WAASWA KUZINGATIA NIDHAMU


Juma la wadau wa Elimu Mkoa wa Dodoma limehitimishwa kwa viongozi mbalimbali  wa Mkoa wa Dodoma kuzungumza na kushiriki chakula cha mchana na wanafunzi wa Shule za kidato cha sita za Mkoa huo.

Kwa nyakati tofauti akiwa katika shule ya Sekondari ya wavulana Kongwa na Shule ya wasichana Kibaigwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewaasa wanafunzi hao kuendelea kudumisha nidhamu hususani katika kipindi hiki wanachojiandaa na mitihani yao na kuachana na marafiki wasiofaa ambao watawasababishia matokeo yatakayogharimu maisha ya ndoto zao.

"Tunataka alama A zenye hapa kuna wenzenu wamechafua jina la Shule na nyie mliopo hapa tunategemea nyie mtabadilisha sura hii ambayo sio njema kwa Mkoa, acheni tabia ya kufuata mkumbo kwa kushawishiana mambo yasiyofaa kwasababu kila mtu ana ndoto yake na kila moja atarudi nyumbani kwao kivyake na usipokuwa makini utaharibu maisha yako kwa mikono yako mwenyewe kwasababu tuu ya ushawishi usiofaa kutoka kwa marafiki zenu.

"Lazima muamue kuachana na baadhi ya mambo na kufuata miongozo yenu na kufanya bidii ili kujitofautisha na wengine na kuongeza ufaulu wenu na kujenga dhana nzuri ya shule Bora ni lazima muwe na ufaulu bora na Shule hii ambayo nyie ndio waanzilishi itapata sifa nzuri na sisi kama Mkoa tunayo matarajio kutoka kwenu kupitia matokeo mazuri mtakayotuletea," ameasa Senyamule

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon amewataka wanafunzi hao kuendelea  kujitunza vizuri  kwa kujiweka bize na masomo na shughuli za kielimu ili kuepukana na vishawishi mbalimbali vitakavyowafanya kupata ufaulu usiofaa na kujenga picha mbaya ya shule yao.

Kwa upande wake ofisa Elimu Mkoa  Mwl. Vincent Kayombo amesema Mkoa wa Dodoma unaendelea na maandalizi ya kuhakikisha Mkoa unapata matokeo mazuri katika mitihani ya kidato cha sita inayotarajiwa kufanyika kuanzia Mei 6, Mwaka huu.

Aidha Mwl.Kayombo ameweka bayana kuwa Mkoa umefanya maandalizi ya kuhakikisha wanafunzi wa shule zenye kidato cha sita za Mkoa huo wanashiriki chakula cha mchana na viongozi mbalimbali ikiwa ni katika kuwahamasisha, kuwatoa hofu na kuwajengea ujasiri wanafunzi hao katika kuelekea mitihani yao ya kuhitimu ngazi hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon amewataka wanafunzi hao kuendelea  kujitunza vizuri  Kwa kujiweka bize na masomo na shughuli za kielimu ikiwemo michezo ili kuepukana na vishawishi mbalimbali vitakavyowafanya kupata ufaulu usiofaa na kujenga picha mbaya ya shule yao.

KATA YA LUPETA WALILIA MAJI

Wananchi wa Kijiji Cha kata Lupeta wilaya ya Mpwapwa Jijini Dodoma  wameiomba serikali kuwapelekea huduma ya maji ili kukabili changamoto hiyo.

Hayo yamebainishwa tarehe 26 Machi 2024 wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Mpwapwa Yohana Malogo kukagua uhai wa Jumuiya, kusajili wanachama wapya
 na kuhimiza ulipaji wa ada.

Walisema kuwa kilio cha maji katika Kata yao imekuwa ni changamoto kiasi cha kushindwa kujua tatizo hilo litaisha lini na serikali inampango gani kwao ili kukabili hali hiyo.

Kwa upande wake Fundi Mkuu wa Maji Geogre Francis Theophil amesema kuwa wapo baadhi ya wananchi wanakata mabomba ya maji usiku bila sababu yoyote kiasi Cha kwamba wanakwamisha swala la maji kupatikana Katika Kijiji hicho.

Theophil amesema kuwa kuna changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu kukata mabomba hali inayosababisha maji kumwagika chini.

Naye Diwani ya Kata ya Lupeta Sospeter Moonho amewahakikishia wananchi mradi wa maji tiririka kufika mwezi wa nne utaenda ili kusaidiia kumtua mama ndoo kichwani pamoja na kuwahakikishia wananchi pia wanaenda kuanza ujenzi wa jengo la zahanati.

Moonho amesema kuwa atahakikisha ujenzi wa jengo la zahanati linakamilika na kama hajakamilisha aulizwe.

Kwa upande wake Mwenyekiti umoja wa Vijana wa Chama Cha mapinduzi ( UVCCM) Yohana Malogo amewataka viongozi wa kata hiyo kuhakikisha mifuko iliyokopeshwa irudidishwe na ujenzi uanze na amewaomba kisima kijengwe kwenye kata hiyo.

Malogo amesema kuwa wanaenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wahakikishe wanawasaidia wananchi na kiasi cha fedha kilichopo ujenzi uanze kwani hakuna sababu kuweka fedha wakati wote huku wananchi wakitaabika.

Lengo ya ziara hiyo ya mwenyekiti wa UVCCM ni kukagua uhai wa Jumuiya, kukagua madaftari ya wanachama, kusajili wanachama wapya na ulipaji wa ada, kuhamasisha kufanyika semina kwa viongozi wa kata na Mitaa pamoja na kikao cha ndani na wanachama.