Na Mwandishi Wetu Dodoma
SHIRIKA la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekanusha Taarifa zilizokua zikisambaa hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii hususan Twitter na Instagram kuhusu mikataba ya mafunzo ya kazi kwa vijana zaidi ya 400 ilivunjwa bila kufuata utaratibu ikiwa imebaki mwaka mmoja kuisha kwa mikataba hiyo.
Akizungumza na Wandishi wa habari Jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania(TASAC) Kaimu Abdi Mkeyenge amesema taarifa zilizozidi kusambaa ni pamoja na vijana kufanya kazi bila bima ya afya na kwamba ilitoa rushwa kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) katika mashauri ya kazi yaliyofunguliwa na vijana hao ili haki isitendeke.
Mkeyenge amesema kuwa mwezi Julai, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania kwa kufuta majukumu ya kipekee ya uwakala wa meli, uhakiki wa mizigo, udhibiti wa nyaraka na kupunguza wigo wa jukumu la kufanya uwakala wa forodha katika bidhaa zilizokuwa zinagombolewa na kuondoshwa na TASAC.
"TASAC ilikuwa ikitekeleza majukumu hayo kupitia vijana waliokuwa wameajiriwa moja kwa moja pamoja na waliokuwa wakifanya mafunzo ya kazi lakini kufuatia mabadiliko hayo Agosti 11 mwaka 2022 TASAC ilivunja mikataba ya mafunzo ya kazi kwa jumla ya vijana 209 waliokuwa wakifanya kazi za uhakiki wa shehena na si zaidi ya 400 kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii,"amesema Mkeyenge.
Amesema kuwa vijana hao waliandikiwa barua kuwa mikataba yao haitahuishwa tena ifikapo tarehe 30 Agosti, 2022 kutokana na merekebisho ya Sheria ambayo yamesababisha baadhi ya majukumu ya TASAC kufutwa na kuhamia sekta binafsi.
"Kwa mujibu wa masharti ya mikataba, TASAC ilikuwa inawapa mkataba ya miezi mitatu na kuongeza muda kila ilipoonekana inafaa kutokana na utendaji kazi wa mtu,"amesema Mkeyenge.
Aidha, mikataba ilikuwa imeainisha utaratibu wa namna ya kuvunja mikataba ya mafunzo kazi na ndiyo utaratibu uliotumika kuvunja mikataba hiyo.
"Kwa kuwa vijana wanaolalamika walikuwa kwenye mafunzo kazi na siyo waajiriwa wa moja kwa moja, TASAC kama taasisi nyingine yoyote ya Serikali haina wajibu wa kuwakatia bima ya afya vijana inaowachukua kwa mafunzo kazini kwani stahiki zao zimeainishwa kwenye Muongozo wa Kitaifa wa Mafunzo Kazini uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu,"amesema Mkeyenge.
Ameongeza kuwa TASAC ni taasisi ya Serikali inayosimamiwa na Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali, hivyo basi mashauri yake kisheria yanasimamiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikiwa ni pamoja na shauri hilo na kuwahakikishia TASAC haijatoa na haiwezi kutoa rushwa yoyote kwa CMA ili kuzuia haki isitendeke kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii.
"Kati ya vijana 209 waliofutiwa mikataba yao, ni vijana 41 tu ambao hawakuridhika na maamuzi hayo na Vijana 32 kati ya vijana 41, shauri lao lilifutwa na CMA kwa kuwa liliwasilishwa nje ya muda, hivyo ni vijana 9 tu ambao shauri lao dhidi ya TASAC lilipokelewa na lipo katika Tume ya Usuluhisi na Uamuzi vijana 168 waliobaki hawakupinga uamuzi wa TASAC wa kuvunja mikataba yao kutokana na mabadiliko ya Sheria ambayo yalikuwa ni nje ya uwezo wa Shirika,"amesema Mkeyenge.
Amebainisha kuwa suala hilo lipo kwenye chombo cha maamuzi kisheria na TASAC haipaswi kulizungumzia shauri hilo lakini ilionekana ni busara kulitolea ufafanuzi wa kilichofanyika kwa upande wa TASAC na kuacha hatua za maamuzi zinazoendelea kuchukua mkondo wake.
"TASAC kama Shirika la Umma linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa na Serikali, hivyo linatoa wito kwa Umma kuwa na subira wakati Tume inapoyafanyia kazi mashauri hayo,"amesema Mkeyenge.