Thursday, August 3, 2017

KIJANA AIGIZA SAUTI YA KIKE AVAA DERA NA HIJABU BODABODA AINGIA MKENGE


Na John Gagarini, Kibaha

KIJANA mmoja anayekadiriwa kuwa na miaka (19) mkazi wa Mbagala Maji Matitu amejikuta yuko kwenye wakati mgumu baada ya kukutwa akiwa amevaa nguo za kike aina ya dera na kusababisha taharuki kwa wakazi wa Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa wa Picha ya Ndege Joseph Zambo alisema kuwa kijana huyo alikuwa akiwasiliana na mtu akijifanya kuwa yeye ni mwanamke.

Zambo alisema kuwa kijana huyo alifika kwenye mtaa wake Agosti 2 majira ya sa 4:30 asubuhi akimfuata mtu waliokuwa wakiwasiliana naye kwa njia ya simu ambaye inadaiwa kuwa ni dereva bodaboda.

“Watu hawa walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu na kijana huyo alikuwa akiigiza sauti ya kike na dereva bodaboda alijua fika kuwa aliyekuwa anawasiliana naye ni mwanamke,” alisema Zambo.

Alisema kuwa dereva bodaboda huyo alimwona kijana huyo kupitia ukurasa wake wa facebook ambapo ulipambwa na picha za msichana hali ambayo ilimfanya avutiwe naye.

“Mawasiliano yalianza kama siku tatu zilizopita na walikubaliana na ndipo bodaboda huyo alimwambia njoo Picha ya Ndege Kibaha lakini kijana huyo alipitiliza hadi Kongowe na ilibidi arudi ashukie Picha ya Ndege na alimwelekeza akishuka apande bodaboda ili aende kwake eneo la Sofu,” alisema Zambo.

Aidha alisema kuwa aliposhuka waendesha pikipiki walikuwa wakimfuatilia na wlimwona amevaa dira na usoni kajifunga kitambaa ambacho kiliacha wazi macho tu kama vile ninja akapandishwa kwenye pikipiki na kuanza safari ya kwenda kwa mtu wake.

“Wakiwa njiani upepo ulipuliza na dereva wa bodaboda akashangaa kuona miguu ya kiume lakini amevaa viatu vya kike akashtuka na kugeuza pikipiki kule alikotoka na ndipo madereva bodaboda walipojaa na kuanza kumzonga hali iliyowabidi wamlete ofisini kwangu na ilikuwa tafrani kubwa huku wengine wakitaka kumpiga wakidai ni mwizi wa pikipiki,” alisema Zambo.

Alibainisha kuwa baada ya kumfikisha walimfunua na kukuta kuwa ni mwanaume na kuanza kumhoji ndipo aliposema kuwa alikuja Kibaha kuja kuchukua hela na haikujulikana alikuja kuzichukua hizo fedha kwa njia gani.

“Zogo lilizidi pale huku bodaboda wakitaka kumpiga ndipo ikabidi tuchukue gari na kumpeleka polisi kwa ajili ya usalama wake na kueleza ni kwa sababu gani alijifanya mwanamke na fedha hizo anazichukua kwa njia gani,” alisema Zambo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa atalitolea taarifa tukio hilo baada ya kutoka kwenye msafara wa kiongozi.


Mwisho.   

No comments:

Post a Comment