Thursday, August 3, 2017

WAZIRI NCHEMBA ALIA NA WANAOWASIDIA WAHAMIAJI HARAMU





                                    Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI imesema imefika wakati kuwakamata watu wanaowasaidia kuwalipia faini wanazopigwa wahamiaji haramu mara wanapohukumiwa mahakamani.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alipotembelea ofisi za Uhamiaji mkoa wa Pwani na kusema kuwa watu hao ndiyo wanaosababisha kuendelea kuingia kinyume cha sheria wahamiaji haramu.

Nchemba alisema kuwa nchi imekuwa ikiingia gharama kubwa kuwatunza wahamiaji haramu wanapoingia nchini na nchi kutumia muda mwingi kuhangaika na wahamiaji hao.

“Hii ni mipango kwani wameshafanya biashara hii kama halali na kuona kuwa hata wakiwalipia adhabu za fedha zinazotolewa na mahakama na kufanya wahamiaji hawa kuingia mara kwa mara hivyo wanaokuja kuwalipia nao kamateni, magari wanayosafirishia wahamiaji haramu taifisheni na boti wanazotumia kamateni,” alisema Nchemba.

Alisema inashangaza kuona Watanzania eti wanawalipia faini wanazopigwa kama adhabu baada ya kubainika kuingia nchini bila ya kibali jambo hilo halikubaliki.

“Hii ni biashara ambayo kuna baadhi ya wenzetu wanajihusisha nayo ndiyo maana tatizo hili haliishi na pia kuna baadhi ya watumishi wa serikali nao wanahusika na tutawachukulia hatua kali watakaobainika kushiriki kwenye mtandao huu wa kuwaingiza wahamiaji haramu,” alisema Nchemba.

Aidha alisema kuwa nchi haiwezi kutumia fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya kununulia dawa za wagonjwa mahospitalini, kujenga barabara, kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu na fedha hizo kuzipeleka kuwahudumia wahamiaji haramu jambo hilo hatutakubali liendelee.

Awali Ofisa Uhamiaji mkoa Plasid Mazengo alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni upungufu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja usafiri na boti kwa ajili ya kudhibiti wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakitumia bandari ya Bagamoyo ambayo ina vipenyo vingi vya kuingilia nchini.

Mazengo alisema kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa wakalimani kwa ajili ya kutafsiri lugha za Kihabeshi na upungufu wa watumishi kwenye baadhi ya wilaya.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment