Monday, August 7, 2017

NETIBOLI PWANI WACHAGUANA


Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA cha Netiboli mkoa wa Pwani kimefanya uchaguzi wa kuwachagua viongozi wake ambao wataongoza kwa kipindi cha miaka minne ambapo Fatuma Mgeni amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika mjini Kibaha na kusimamiwa na kamati ya michezo ya mkoa ikiongozwa na ofisa michezo wa mkoa huo Grace Bureta ulimrudisha madarakani mwenyekiti huyo.

Wengine waliochaguliwa ni makamu mwenyekiti Faraji Makale, katibu ni Steven Mzee, katibu msaidizi ni Rehema Kiharaza, mweka hazina Octavian Chuma.
Kwa upande wa wawakilishi mkutano mkuu taifa ni Ndimbumi Ifuge, Lonjin Mzava, Omega Shuma, Witnes Kitereja na Grace Paschal.

Akiwaasa viongozi waliochaguliwa ofisa michezo huyo aliwataka viongozi hao kuwa kitu kimoja na kushirikiana ili kuinua mchezo huo kwenye mkoa kwa manufaa ya wachezaji wa mchezo huo.

Bureta alisema kuwa uongozi imara ndiyo utakaofanikisha kukabili changamoto mbalimbali zilizopo za kuuboresha mchezo huo ambao ulikuwa maarufu kwenye mkoa wa Pwani kwa miaka ya nyuma.

“Muwe na maamuzi ya pamoja na si ya mtu mmoja na kusitokee akafanya kama ni mali yake hali ambayo itasababisha mchezo huo ushindwe kupiga hatua,” alisema Bureta.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama hicho Fatuma Mgeni alisema kuwa moja ya vitu atakavyovifanyia kazi ni kufanya mafunzo kwa walimu wa mchezo huo ili wajue sheria mpya za mchezo huo ambazo zilifanyiwa marekebisho mwaka 2016 nchini Afrika Kusini.

Mgeni alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa kwa walimu wa mashule, vyuo na kwa wadau mbalimbali wanaoupenda mchezo huo na wanaotaka kuwa walimu wa kufundisha netiboli.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment