Thursday, August 3, 2017

HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAOMBWA KUTENGA FEDHA KWA WATU WENYE ULEMAVU

Na John Gagarini, Kibaha

WADAU wa watu wenye ulemavu kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha wameiomba Halmashauri hiyo kutenga asilimia moja ya mapato ya ndani kwa ajili ya kukabili changamoto za ulemavu.

Hayo yalisemwa na Methew Chungu mwezeshaji wa  mafunzo yaliyoandliwa na Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Kibaha Mjini kwa wadau wa huduma za afya kwa watu wenye ulemavu.

Chungu alisema kuwa mapato hayo yangesaidia kuwapatia huduma mbalimbali watu wenye ulemavu zikiwemo za kiafya, elimu, kiuchumi na huduma nyingine za kiutu.

Naye katibu wa SIVYAWATA Kibaha Mjini Happiness Matagi alisema kuwa kwa sasa changamoto za upataji huduma kwa watu wenye uelemavu zimepungua ambapo kumwona daktari kwa ni bure.

Matagi alisema kuwa kupitia kituo chao cha watu wenye ulemavu kilichopo Kwa Mfipa wanatoa huduma mbalimbali za kiafya hasa kwa wale walemavu wa viungo pamoja na shughuli za ujasiriamali.

“Pale watu wenye ulemavu wanafanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufuma, kushona nguo na mradi wa matofali ambao uko mbioni kuanza lengo kuwakwamua watu wenye ulemavu ili wasijione wanyonge na kuachana na tabia ya kuomba ambayo itawafanya washindwe kujitegemea,” alisema Matagi.

Kwa upande wake mwakilishi wa mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Dk Mariamu Mgaya alisema kuwa watu wenye ulemavu wamekuwa wakisaidia ili kuhakikisha wanapata huduma za afya bila ya usumbufu kwa kuwapa kipaumbele.

Akijibu baadhi ya hoja ofisa mipango wa Halmashauri ya Mji Kibaha Amkauane Ngilangwa alisema kuwa katika bajeti iliyopitishwa watu wenye ulemavu wametengewa kiasi cha shilingi milioni 10.


Ngilangwa alisema kuwa pia wanapatiwa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuta ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi albino ili ngozi zao zisiharibike na fimbo kwa ajili ya wasioona. 

No comments:

Post a Comment