Sunday, August 6, 2017

WATOTO WAFA MTO RUVU MMOJA WA MIEZI MINNE













Na John Gagarini, Chalinze

WATU watatu wakiwemo mtoto wa miezi minne na wa mwaka mmoja wamekufa huku watu wawili wakinusurika kifo baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama kwenye mto Ruvu.

Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa licha ya watu hao kubainika kufa dereva wa mtumbwi huo hajulikani alipo.

Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 5 majira ya saa 4:00 asubuhi wakati watu hao walipokuwa wakijaribu kuvuka mto kutoka Vigwaza kwenda Mlandizi kwenye mto Ruvu wilaya ya kipolisi Chalinze.

“Ajali hiyo imepoteza maisha ya watoto wawili ambao ni Nusrat Haji miezi minne na Feisal Hamza mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu pamoja na Sikuzani Musa (41) ambaye mwili wake bado haujapatikana,” alisema Shana.

Alisema kuwa walionusurika ni Zuwena Ramadhan (29) na Tero Mziray (20) ambapo dereva wa mtumbwi huo hajulikani alipo na inaaminika hakufa maji.

“Chanzo cha mtumbwi huo kuzama bado kinachunguzwa na miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi,” alisema Shana.

Aliwataka wamiliki wa vyombo hivyo kuhakikisha vinakuwa kwenye hali nzuri ili kuepukana na ajali kama hizo ambazo zinapoteza uhai wa watu kutokana na ubovu.

Mwisho.   


No comments:

Post a Comment