Monday, August 14, 2017

WATATU WAFA PWANI


Na John Gagarini, Kibaha

WATU watatu wamefariki dunia na wengine 11 wamejeruhiwa kutokana na ajali mbili tofauti zilizotokea mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana imesema kuwa matukio hayo yalitokea wilaya za Kisarawe na Bagamoyo.

Kamanda Shana amesema kuwa tukio la kwanza lilitokea Agosti 10 majira ya saa 11:15 jioni eneo la Mwambisi wilaya ya Kisarawe basi dogo aina ya Eicher lenye namba za usajili T192 DDD likitokea Masanga kwenda Buguruni Jijini Dar es Salaam liliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku 11 wakijeruhiwa.

Amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni breki kushindwa kufanya kazi na kusababisha gari hilo kupoteza mwelekeo na kupinduka na kusababisha kifo cha mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (60) ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.

Amebainisha kuwa majeruhi wawili Fatma Hamis (35) aliyeumia kifuani na John Clement aliyevunjika mguu wa kulia wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Aidha amesema kuwa baada ya gari hilo kupinduka liligonga mzinga wa nyuki ambao waliingia kwenye basi na kujeruhi watu tisa ambao wamelazwa kwenye hospitali ya Kisarawe na dereva wa gari hilo alikimbia baada ya tukio hilo ambapo jeshi hilo linamtafuta.

Katika tukio la pili dereva wa pikipiki na abiria wake wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari.

Shana amesema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 13 majira ya saa 11:40 jioni ambapo pikipiki hiyo aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 315 BLM iliyokuwa ikiendeshwa na Ally Seif (19) mkazi wa Kerege iligongana na gari aina ya Mitsubishi Fuso likitokea Dar es Salaam kwenda Bagamoyo likiendeshwa na dereva ambaye hakufahamika.

Amebainisha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa bodaboda kulipita gari lililokuwa mbele yake kwa kasi bila ya kuchukua tahadhari na kugongana uso kwa uso na kusababisha vifo hivyo vya dereva na abiria wake Mohamed Rajabu (18) mkazi wa Kerege    

Amewataka wamiliki wa magari kufanya matengenezo ya magari yao pindi yanapokuwa na hitilafu na madereva wasikubali kuendesha magari mabovu pia wafanye ukaguzi wa kina katika magari yao kabla ya kuanza safari kwani ubovu wa magari huchangia ajali kwa kiasi kikubwa.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment