Thursday, August 3, 2017

MWIGULU ATAKATAARIFA ZA WATANZANIA ZIUNGANISHWE MTANDAONI


                                     Na John Gagarini, Kibaha

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba ametaka taarifa za Watanzania ziunganishwe kwenye mtandao tangu wanapozaliwa ili wasipate usumbufu wa kupata barua za utambulisho wanapotaka huduma mbalimbali.

Aliyasema hayo wakatia alipotembelea jengo jipya la kisasa la vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kusema hakuna haja ya mtu kila anapoomba huduma fulani awe na barua ya utambulisho toka kwenye mtaa anaoishi.

Nchemba alisema kuwa kwa sasa mifumo inakwenda kisasa na mtu anapotaka huduma fulani wanakwenda kwenye mtandao na kupata taarifa zote za muhusika.

“Mfano mtu anataka paspoti, leseni, kusajili biashara, laini za simu na huduma nyingine hapaswi kuwa na mabarua kwa kila huduma anayoitaka bali wanaangalia tu kwenye mifumo hii na kuzipata taarifa za mtu,” alisema Nchemba.

Alisema kuwa uunganishaji wa taarifa za wananchi na kuwa na utambulisho wa aina moja utasaidia kupata taarifa na itaonyesha kama ni dereva kujua ni makosa gani aliyokwisha kuyafanya hivyo ni rahisi kumdhibiti.

 “Mifumo hii ya kimtandao itasaidia sana kuhuisha huduma nyingi ambazo mtu anapaswa kwenda kwenye ofisi mbalimbali bali anaweza kutumia ofisi moja kupata taarifa zozote zinazotakiwa,” alisema Nchemba.

Aidha alisema kuwa taarifa hizo zitasaidia hata kupunguza kuwabaini raia wageni ambao wanaingia nchini kinyemela ambao hawaeleweki wako kwa ajili ya madhumuni gani.

Naye kaimu mkurugenzi wa uzalishaji wa Vitambulisho Alfonce Malibiche alisema kuwa ujenzi huo umefikia hatua za mwisho na wanatarajia utakamilika mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao.

Malibiche alisema kuwa mara ujenzi huo utakapokamilika vitambulisho vya uraia vitakuwa vikizalishwa hapo ambapo kwa sasa ujenzi huo uko mwishoni.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka aliomba serikali ikitoa ajira izingatie wakazi wa wilaya hiyo na mkoa wa Pwani ili iwe manufaa kwa kujengwa ofisi hizo.

Koka alisema kuwa uzingatiaji wa kuajiri vijana na wataalamu kutoka kwenye eneo husika utaleta manufaa makubwa kwa mkoa huo ambao unainukia kwa kasi katika uwekezaji ukiwemo wa viwanda.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment