Sunday, August 6, 2017

WAETHIOPIA 72 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUINGIA NCHINI BILA YA KIBALI

Moja ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni wahamiaji haramu kutoka nchi ya Ethiopia akiwahudumia wenzake kwa kuwapa mikate kwenye kituo cha Polisi wilaya ya Kipolisi ya Chalinze baada ya kukamatwa huko Ruvu Vigwaza wilayani Bagamoyo mkoani Pwani

 Moja ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni mhamiaji haramu toka nchi ya Ethiopia akiwekewa uji pembeni ni askari akisubiri kupewa uji kwa ajili ya kuwapa watuhumiwa hao.

 Baadhi ya waethiopia wanaotuhumiwa kuingia nchini bila ya kibali wakipata kifungua kinywa cha uji.

 Askari akiwapatia mikate watu wanaotuhumiwa kuingia nchini bila ya kibali raia wa Ethiopia wakipata uji.

 Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Jonathan Shana akiwa mbele ya watu ambao wanatuhumiwa kuwa ni wahamiaji haramu  kutoka nchi ya Ethiopia ambao walikamatwa mkoani humo.
Na John Gagarini, Chalinze

HUKU Serikali ikiwa inaweka mikakati ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu hapa nchini Jeshi la polisi mkoa wa Pwani limewakamata wahamiaji haramu 72 kutoka nchi ya Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kituo cha wilaya ya Kipolisi ya Chalinze kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa wahamiaji hao walikuwa safarini kwenda Afrika ya Kusini.

Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 5 majira ya saa 3:30 asubuhi kwenye Pori la Ranchi ya Taifa (NARCO) kata ya Vigwaza wilaya ya Kipolisi ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo.

“Mbali ya wahamiaji hao haramu pia tunamshikilia Rajabu Hitaji (30) mkazi na mfanyabiashara wa Vigwaza baada ya msako mkali uliofanywa na makchero wa jeshi la polisi baada ya kupata taarifa kuwa kuna wahamiaji haramu wameingia bila ya kibali,” alisema Shana.

Alisema kuwa wahamiaji hao haramu baada ya kugundua kuwa kuna gari la polisi linawafuatilia waliingia kwenye hifadhi hiyo kwa lengo la kujificha lakini msako mkali uliofanywa uliweza kuwabaini na kukamata kundi la kwanza la watu 63 ambao walikaa sehemu ambayo gari haliwezi kufika.

“Baada ya kuwakamata wahamiaji hao haramu kundi la kwanza askari waliendelea na msako ambapo waliwakamata wahamiaji wengine tisa waliokuwa wakijaribu kutaka kutoka kwenye pori hilo,” alisema Shana.

Alisema kuwa wahamiaji hao haramu wanatarajiwa kukabidhiwa idara ya Uhamiaji kwa ajili ya hatua za kisheria pamoja na mfanyabiashara aliyekamatwa ambaye anatuhumiwa kuwasafirisha.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment