Na John Gagarini, Chalinze
NCHI ya Pakistani imesema kuwa itaendelea kusaidia miradi mbalimbali ya
maendeleo hapa nchini ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa nchi hiyo na
Tanzania.
Hayo yalisemwa na Balozi wa Pakistani hapa nchini Amir Khan wakati wa
sherehe za kupokea majengo ya madarasa ya Shule ya Msingi Pakistani Mtete
yaliyokarabatiwa na marafiki wa Pakistani.
Khan alisema kuwa nchi yake imekuwa na miradi mbalimbali ya kimaendeleo
hapa Tanzania na hiyo inatokana na urafiki uliopo baina ya nchi hizo.
“Tumekuwa na miradi mingi hapa Tanzania na tutaendelea kushirikiana kama
walivyofanya wenzetu na kujitolea kukarabati shule hii,” alisema Khan.
Alisema kuwa miradi kama huo uliofanyika kwenye shule hiyo ni fedha
ambazo walitoa marafiki wa Pakistani kwa ajili ya kuhakikisha sekta ya elimu
inaboreka.
“Suala la elimu ni muhimu kwa watoto ambao baadaye tunatarajia watakuwa
wataalamu wazuri hivyo lazima kuwawekea mazingira mazuri ya kusomea,” alisema
Khan.
Aidha aliwataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya shule hiyo ili
ukarabati uliofanyika uwe na maana hata mazingira yanaendelea kuwa mazuri.
“Kuhusu uzio kwenye shule hiyo alisema kuwa atapeleka ombi hilo kwa marafiki
wa Pakistani ili walifanyie kazi kama ilivyoombwa na Mbunge wa Jimbo la
Chalinze Ridhiwani Kikwete,” alisema Khan.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete aliwapongeza Marafiki hao wa
Pakistani kwa kuisaidia shule hiyo na kusema kuwa watahakikisha wanenzi
ukarabati huo kwa kuitunza miundombinu ya shule.
Ridhiwani alisema kuwa jambo watakalolifanya ni kuhakikisha eneo hilo
linapimwa na kuwekewa mipaka ili kukabiliana na wavamizi.
“Tutahakikisha linapimwa na kuwekewa mipaka yake kwani baadhi ya watu
wamekuwa wakivamia maeneo yakiwemo yale ya taasisi,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa pia watahakikisha miundombinu mingine inatengenezwa ili
kuifanya shule hiyo kuwa na mazingira mazuri ya utoaji elimu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment