Na John
Gagarini, Kibaha
JESHI la
Polisi limesema kuwa bado linaendelea kumshikilia kijana wa kiume mkazi wa
Mbagala Jijini Dar es Salaam ambaye alivalia mavazi ya kike ikiwemo dera hijabu
na kuficha sura yake kwa kuva nikabu.
Kamanda wa
Jeshi la Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa kijana huyo alikamatwa
Agosti 2 maeneo ya Picha ya Ndege barabara ya kuelekea Magereza huku akiwa
amevaa mavazi hayo.
Shana alisema
kuwa kwa sasa jeshi hilo bado linamshikilia kijana huyo kwa ajili ya mahojiano
ili kubaini mtandao anaoshirikiana nao kwenye matukio ya uhalifu.
“Kijana huyu
tulimkamata baada ya kumwekea mtego uliowekwa na makachero wetu waliokuwa
wamepata taarifa kutoka kwa wasiri waliokuwa wanamtilia mashaka na walifanikiwa
kumkamata akiwa kwenye bodaboda akielekea maeneo ya Magereza,” alisema Shana.
Alisema kuwa
hadi sasa bado hawajajua kijana huyo alikuwa na lengo gani la kuvaa nguo hizo
za kike hali ambayo hadi sasa bado haijafahamika hasa alidhamiria nini.
“Hadi sasa
tunaendelea kumhoji kujua ni kwanini avae mavazi ya kike na tunawashukuru
wananchi na wasiri wetu kwa kuendelea kutupa ushirikiano wa kufanikisha
kukamatwa kwa wahalifu,” alisema Shana.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment