Thursday, February 25, 2016

WAZIRI SIMBACHAWENE AIKATALIA KEC COTC KUWA CHUO KIKUU

Na John Gagarini, Kibaha
WAZIRI wa Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene amelitaka Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kutokibadili Chuo cha Waganga Wasaidizi (COTC) kuwa Chuo Kikuu ili lisiharibu malengo ya chuo kusomesha watu wenye elimu ya kawaida.
Simbachawene aliyasema hayo alipotembelea Shirika hilo hivi karibuni na kusema kuwa ndiyo sababu chuo hicho hakikuingizwa kwenye Taasisi ya elimu ya juu kwani malengo yake ni kusomesha watu ambao ni wa ngazi ya kati.
Alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na hali ya kila chuo kutaka kuwa chuo kikuu hali ambayo itasababisha kusiwe na wataalamu wa ngazi ya kati ambao wameonekana kuwa ndiyo wawajibikaji wakubwa.
“Kama kila chuo au taasisi itakuwa na malengo ya kuwa chuo kikuu kuna hatari ya kuwapoteza wasomi wa ngazi ya kati kwani endapo kila mtu atakuwa amesoma chuo kikuu hakutakuwa na watu wa kufanyakazi kwani kila mtu atatakuwa mtawala,” alisema Simbachawene.
Alisema kuwa chuo hicho kilianzishwa kwa malengo ya kuwapatia elimu watu wa vijijini lakini kikishafanywa chuo kikuu wananchi wenye elimu ya kati hawatapata nafasi ya kusoma hivyo malengo ya kuisaidia jamii hayataweza kufikiwa.
“Tunashindwa kupata wagunduzi kwani wanakuwa ni watu wenye elimu ya kawaida sana kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea hawa ni watu waliosoma elimu ya kawaida na wengine wanatoka vijijini hivyo na hapa ni sehemu ya kuanzia lakini tukikibadilisha na kuwa chuo kikuu ni sawa na kuvunja daraja ambalo watu wamekuwa wakitumia kuvukia kwenda mbele,” alisema Simbachawene.
Aidha alisema kuwa kuna tatizo la wataalamu wa kati kutokana na watu wengi kuiacha elimu ya kati na kutaka kupata elimu ya juu hivyo kumekuw ana pengo hapo katikakati pia wazingatie malengo ya kuanzishwa chuo hicho ambacho zamani kilijukana kama chuo cha maendeleo ya waganga vijijini.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment