Thursday, February 25, 2016

WAJERUMANI WAFAGILIA ELIMU BURE TANZANIA

Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya Raia wa nchi ya Ujerumani waliokuja nchini kwa ajili ya kufanya shughuli za kujitolea kwa jamii wilayani Kibaha mkoani Pwani wameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuanzisha utaratibu wa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha wakati wa zoezi la kusafisha eneo la kujenga shule ya sekondari ya mtaa wa Mbwate raia hao walisema kuwa utaratibu huo unatoa fursa kwa watoto wengi waliofikia umri wa kwenda shule kupata nafasi hiyo.
Laura Pommerenke alisema kuwa utoaji wa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari utalifanya Taifa la Tanzania kuwa na watoto wengi watakaokuwa wemekwenda shule tofauti na ilivyokuwa zamani.
“Utaratibu wa elimu bure ni mzuri kwani hata kule kwetu ambako watu wanauwezo wanafunzi wanapata elimu bure hali ambayo inawafanya watoto kupata elimu inayostahili kwa wakati na kuondokana na watu kutokuwa na elimu,” alisema Pommerenke.
Alisema kuwa msingi wa elimu ya awali ukiwekwa utasaidia nchi kukabiliana na tatizo la watoto wa Tanzania kukosa elimu hali ambayo itazidi kuongeza umaskini lakini wakipata elimu watakuwa na uwezo wa kujitegemea.
Naye Marie Vogel alisema kuwa alisikia kuwa elimu ya Msingi na Sekondari ili kuwa na gharama jambo ambalo liliwafanya watoto wengi washindwe kwenda shule hivyo kuwafanya watoto wengi kuwa mitaani au kuanza maisha kabla ya wakati wao.
Vogel alisema kuwa serikali ya Tanzania inapongezwa kutokana na kuchukua maamuzi hayo ya kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari kwani mpango huo utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo Abdala Mtandio alisema kuwa mpango wao wa kujenga shule ya sekondari kwenye mtaa wao umezingatia tatizo la watoto wengi kusoma mbali na kujikuta wakitumia mwingi njiani.
Mtandio alisema kuwa malengo yao ni kujenga madarasa manne ya kuanzia ili wanafunzi waanze kusoma hapo na wanahitaji kiasi cha shilingi milioni 50 za kuanzia pia wamewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment