Tuesday, February 16, 2016

MASHAMBAPORI YARUDI SERIKALINI


Na John Gagarini, Kibaha
KATIKA kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kuwanyanganya watu wasioendeleza mashamba kwenye wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imerudisha mashamba 17 serikalini ambayo yatatumika kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba wakati wa kuzindua Jukwaa la Uwajibikaji kwa Asasi ya Kitaifa ya Ushirikiano wa Maendeleo  ya Vijana (YPC) ya mkoa wa Pwani na kusema kuwa mashamba hayo pia yatatumika kwa ajili ya makazi.
Kihemba alisema kuwa mashamba hayo yalikuwa kero kwa wananchi kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu na wamiliki licha ya kutakiwa kuyaendeleza kisheria lakini wameshindwa na kuyafanya mapori makubwa.
“Baadhi ya mashamba yamerudishwa serikalini kama tulivyoagizwa na tutahakikisha tunayapima kwa ajili ya viwanda ili kuweza kuimarisha uchumi wa wakazi wa wilaya ya Kibaha pia sehemu yatapimwa kwa ajili ya makazi,” alisema Kihemba.
Alisema kuwa maeneo hayo yaliyorejeshwa hayapaswi kuvamiwa kwani kuna taarifa baadhi ya watu wameanza kuyavamia mashamba hayo jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwani yatatumiwa kwa mipango itakayokuwa imepangwa na si kwa watu kuyavamia.
“Ni marufuku watu kuyavamia maeneo hayo ambayo yalirejeshwa serikalini na kwa wale watakaojenga nyumba zao zitabomolewa wanachotakiwa ni kusubiri utaratibu utakaowekwa na serikali na si kujichukulia kinyume cha sheria,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa kwa kuwa serikali ya awamu ya tano imepania kuinua uchumi wa Watanzania kupitia viwanda ili wawe na uchumi wa kati ni vema na wao wakaunga mkono mpango huo kwa kuanzisha viwanda kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment