Na John Gagarini, Kibaha
Akizungumza mjini Kiabaha kwwenye Jukwaa la Uwajibikaji kwa
asasi isiyo ya kiserikali ya kitaifa ya ushirikiano wa Maendeleo kwa Vijana (YPC)
mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa mashirika kama hayo endapo
yatajihusisha na siasa yatafutwa.
Kihemba alisema kuwa mashirika hayo yalianzishwa kwa lengo la
kuwasaidia wananchi katika masuala ya kimaendeleo na si kujihusisha na siasa
kama baadhi yanavyofanya kwa kujiingiza kwenye siasa.
“Msijiingize kwenye siasa bali mnapaswa mshirikiane na
serikali katika kukabiliana na changamoto lakini endapo mtaingia kwenye siasa
mnaweza kuathiri utendaji kazi wenu na tutayafuta yale ambayo yanajiingiza
kwenye siasa kwani vyama vya siasa ndiyo vinapaswa kushiriki siyo nyie kwani
kazi yenu ni maendeleo,” alisema Kihemba.
Alisema kuwa shirika hilo limefanya kazi kubwa kuwahamasisha
vijana kushiriki kwenye kuwania nafasi za uongozi pamoja na kuwajengea uwezo wa
uwajibikaji ni vema wakaendelea na shughuli za kimaendeleo kwa kuwaonyesha
wananchi fursa za maendeleo kwani wao ni wabia.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi mwenyekiti wa bodi ya YPC Mkuku
Mlongecha alisema kuwa asasi yao haijihusishi na masuala ya kisiasa bali ni
kuwajengea uwezo vijana kushiriki kwenye shughuli za maendeleo pamoja na uongozi.
Mlongecha alisema kuwa malengo mengine ni kuwajengea uwezo wa
kisiasa, kijamii, uchumi, kujitolea pamoja na mafunzo kwa vijana ambapo
asilimia zaidi ya 70 ya madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji ni
vijana.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment