UMOJA wa Wafanyabiashara wa Mazao ya Misitu Wilayani Kisarawe mkoani Pwani (UWAMAMI) wameomba suluhu na Halmashauri ya Wilaya ili waache mgomo wa kufanya biashara hiyo kwa kurejeshewa fedha zao za faini ambazo walitozwa kimakosa.
Wafanyabiashara hao walisema kuwa wataachana na mgomo huo endapo Halmashauri hiyo hiyo itawarudishia fedha zao kiasi cha zaidi ya shilingi milioni nne ambazo wafanyabiashara hao walipigwa kinyume cha taratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari Makamu Mwenyekiti wa umoja huo Mohamed Dikata alisema kuwa mgomo huo utaendelea hadi pale Halmashauri itakapowarejeshea fedha zao kwani hali hiyo imeathiri biashara zao hasa ikizingatiwa walikiri kuwa walifanya makosa katika upigaji fani huo kwa wafanyabiashara ambao walizidisha mzigo wa mazao ya misitu walipokuwa wakiitoa mashambani.
“Sisi tunatoa huduma kwa wananchi hivyo tunaomba Halmashauri warudishe fedha hizo ambazo ni sehemu ya mitaji yetu na tumejaribu kukaa mara kadhaa bila ya kufikia muafaka kwani wao wanataka kutulipa kidogo kidogo fedha zetu jambo ambalo hatujaliafiki tulipigwa faini ambapo wengine walipigwa faini na kufikia zaidi ya milioni moja na kutoa fedha taslimu kwani nini wao warejeshe kwa mafungu kwani sehemu ya fedha tulizotoa ni za biashara hivyo kuyumbishwa katika shughuli zetu za kibiashara," alisema Dikata.
Aidha alisema kuwa wanataka watumishi wa Halmashauri waliohusika waondolewe kwani wamekiuka taratibu za kazi zao kwa kuwalipisha faini zisizostahili kwani si mara yao ya kwanza hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Walitupiga faini ya shilingi 16,000 kwa kila gunia badala ya shilingi 1,600 kwa gunia ambalo linakuwa limezidi na sisi hatukatai kulipa faini ambayo ni halali tunachopinga ni kuzidishiwa mara 10 zaidi ya faini halali,” alisema Dikata.
Jitihada za kumpata mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe hazikufanikiwa kwani alikuwa nje ya ofisi kikazi ambapo kaimu wake naye hakupatikana hata hivyo ofisa Mipango wa Patrick Alute alikiri kuwa na tatizo hilo na kusema kuwa mazungumzo yanaendelea baina ya wafanyabiashara hao.
Alute alisema kuwa Halmashauri inaendelea na mazungumzo ili kufikia muafaka, umoja huo hujihusisha na biashara ya uuzaji wa mkaa pamoja na kuni ambapo gunia moja hulipiwa kiasi cha shilingi 20,000 kama ushuru wa Halmashauri.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment