Sunday, February 7, 2016

WANANCHI WATAKIWA KUTOWAHIFADHI WAGENI

Na John Gagarini, Kibaha
IDARA ya Uhamiaji Mkoani Pwani imewataka  wananchi kutokubali kukaa na wageni ambao si raia Watanzania kwani ni kinyume cha taratibu na endapo watabainika watachukulia hatua za kisheria kwa kuwatunza wageni.
Hayo yalisemwa na Naibu Kamishna wa Idara hiyo Grace Hokororo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisni kwake mjini Kibaha na kusema kuwa kuna watu wanaishi na wageni jambo ambalo ni kosa kisheria.
Hokororo alisema kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiishi na wageni majumbani mwao wengine wakiwa wamewapangisha, wamewaajiri au kuwapangisha kwenye nyumba zao kama Raia wa Tanzania bila ya kufuata taratibu.
“Mgeni yoyote anapoingia nchini anapaswa kufuata taratibu na lazima serikali au idara hivyo watu wanaokaa nao au kufanya nao shughuli yoyote bila ya kufuata taratuibu za nchi ni kosa na endapo wanagundua kuwa siyo raia wanapaswa kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe kwa mhamiaji haramu,” alisema Hokororo.
Alisema kuwa changamoto inayowakabili ni uchache wa watumishi hali ambayo inawafanya washindwe kuwadhibiti wahamiaji haramu hao ambao wamekuwa wakileta athari nyingi kwa raia  endapo atakaa kinyemela bila ya kufuata taratibu.
“Kuna athari mbalimbali zinazotokana na Raia wa nje kuishi bila ya kibali ikiwa ni pamoja na kunyakua rasilimali kama vile mashamba na vitu vingine lakini akiishi kwa kufuata taratibu kuna namna ya kupewa rasilimali bila ya kumwathiri mwenyeji,” alisema Hokororo.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine ni mkoa kutawanyika na njia za kuingilia ni nyingi kwa kupitia kwenye Bahari ambako hakuna vyombo vya kufanya doria kwenye bandari ambazo nyingine ni bubu ambazo zinatumika kama milango ya kuingilia.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment