Na John Gagarini, Kibaha
MAWAKALA wote wanaokusanya mapato ya Halmashauri ya Mji wa
Kibaha mkoani Pwani wametakiwa walipe makusanyo yao yote wanayodaiwa na Halmashauri
ndani ya mwezi mmoja.
Agizo hilo lilitolewa jana na mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia
Evarist Ndikilo wakati akifungua baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo
nakusema kuwa ucheleweshaji wa fedha hizo unasababisha Halmashauri kushindwa
kufanya mipango yake ya maendeleo.
Alisema kuwa baadhi ya mawakala wamekuwa wakichelewesha
makusanyo na tozo mbalimbali wanazozitoza toka kwa wananchi kwa niaba ya
Halamashauri hivyo wanapaswa kupeleka malipo hayo kwa wakati.
“Moja ya hoja ambazo zimekuwa zikiwasilishwa na Mkaguzi Mkuu
wa Serikali (CAG) ni kushindwa kukusanya mapato ya ndani ya mawakala kwa wakati
na kukosa mikakati ya kuongeza mapato ya Halmashauri,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa suala lingine ni mikataba inayoingiwa
inakuwa si mizuri na inatoa mwanya kwa wakala kuacha kuwasilisha mapato bila ya
kuchukuliwa sheria kutokana na kuchelesha mapato hayo.
“Pia nashauri madiwani wajiepushe na kuomba zabuni mbalimbali
katika Halamashauri ili kuepuka migongano ya kimaslahi na muweze kuisimamia vizuri
kwani endapo mtakuwa na maslahi hamtaweza kuisimamia hivyo kushindwa kuleta
maendeleo,” alisema Ndikilo.
Aliwataka Madiwani kusimamia fedha za makusanyo ya ndani
zianarudi kwa wananchi kwa kugaramia huduma mbalimbali na miradi ya maendeleo
kwa ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri Leonard Mlowe
alisema kuwa watendaji wa halmashauri wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa
kuwa waadilifu ili kufanikisha maendeleo kwa wananchi yanapatikana.
Mlowe amewataka watendaji hao kuwasimamia mawakala ili wahakikishe
wanawasilisha fedha za makusanyo mbalimbali zinafika kwa wakati ili kuwaletea
maendeleo wananchi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment