Sunday, February 14, 2016

WATAFUTA MILIONI 50 UJENZI WA MADARASA YA SEKONDARI

NA John Gagarini, Kibaha
WAKAZI wa Mtaa wa Mbwate kata ya Msangani wilayani Kibaha mkoani Pwani wanahitaji kiasi cha Shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ya shule ya sekondari kwenye mtaa huo.
Mtaa huo una wanafunzi zaidi ya 500 wanaotoka kwenye mtaa huo kwenda kusoma kwenye shule ya sekondari ya Nyumbu ambayo iko umbali wa kilometa zaidi ya 10 hali ambayo inawapa wakati mgumu wanafunzi hao kutokana na umbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye eneo ambalo wanalifanyia usafi kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo mwenyekiti wa mtaa huo Abdala Mtandio alisema kuwa walikuwa wamelenga kuanza ujenzi mwakani lakini kutokana na wanafunzi wengi wanaotoka kwenye mtaa huo kusoma mbali wameona afadhali waanze na madarasa machache ili kuwasaidia watoto wao ili wasome karibu na wanakoishi.
“Tunaomba wadau watusaidie kupata fedha hizo ili tuanze ujenzi kwani kwa sasa shule ya sekondari ya Kata ya Nyumbu  imeelemewa na wanafunzi hivyo tunaiomba Halmashauri iwapunguzie wanafunzi hao kwenye shule tutakayojenga kwani kwenye mtaa wetu kuna eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari wakati kule hawana eneo la kuongeza madarasa,” alisema Mtandio.
Mtandio alisema kuwa kutokana na serikali kutaka shule kuongeza madarasa kwa zile ambazo zina wanafunzi wengi ni vema Hlamashauri ikaongeza nguvu kwenye ujenzi wa shule ambayo wanataka kujenga ili kupunguza mlundikano wa wanafunzi kwenye shule hiyo ya Nyumbu.
“Tunaomba wadau watusaidie kwani kwa sasa eneo limepatikana kwa ajili ya ujenzi ambalo lina ukubwa wa hekari 10 tumeanza kwa kujitolea kufyeka vichaka na sasa tunajitolea kungoa visiki ambapo pia tunaomba Halmashauri itusaidie greda kwa ajili ya kungoa visiki tuliomba muda mrefu ambapo tathmini ilifanyika na kuonekana kuwa zinahitajika kiasi cha shilingi milioni nane kwa ajili ya greda,” alisema Mtandio.
Kwa upande wake mmoja wa wakazi wa mtaa huo Steven Mwita alisema kuwa malengo ya mtaa wetu ni kuanza ujenzi kuanzia mwezi wanne hivyo wanawaomba serikali na wadau wengine wa maendeleo wawasaidie kwa kuwachangia kwa hali na mali ili wafikie lengo la kujenga shule ya sekondari.
Mwita alisema kuwa matarajio yao ni kufanya ujenzi wa kisasa wa ghorofa ili baadaye wawe na elimu ya juu yaani kidato cha tano na cha sita kwa lengo la kuinua sekta ya elimu kwenye mtaa pamoja na wilaya nzima ya Kibaha

Mwisho.

No comments:

Post a Comment