Sunday, February 14, 2016

MAMA AMFANYIA UKATILI MWANAE WA KAMBO AMVUTA SEHEMU ZA SIRI


Na John Gagarini, Kibaha
SHEILA Husein mkazi wa Janga Kata ya Janga Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani amejikuta matatani baada ya kumpiga mtoto wake wa kambo wa kiume mwenye umri wa miaka (2) na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili ikiwa ni pamoja na kumvuta sehemu zake za siri.
Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa Mtaa wa Janga na Diwani wa kata hiyo Chande Mwalika alisema kuwa mtoto huyo amekuwa akipigwa kila siku kwa fimbo hali ambayo imemfanya awe na makovu mengi mwilini.
Mwalika alisema kuwa moja ya majirani ambaye alishindwa kuvumilia vitendo hivyo Adinani Mkupa nakutoa taarifa hiyo alisema kuwa vitendo vilivyokuwa vikifanywa na mtuhumiwa huyo ni vya kikatili na haviwezi kuvumilika.
“Amekuwa akimchapa mwanae kwa fimbo bila ya kumuonea huruma hali ambayo imemfanya mtoto huyo aharibike mwili mzima kutokana na vipigo hivyo na kibaya zaidi ni pale alipofikia hatua ya kumvuta sehemu zake za siri na hakuna sababu maalumu inayomfanya amwazibu mtoto huyo kwani bado ni mdogo sana na hana uwezo wa kuongea,” alisema Mwalika.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo ilibidi watoe ripoti kwa kwenye uongozi wa kata kwa ajili ya hatua zaidi kwa mtuhumiwa ambaye ni mama wa nyumbani huku mumewe aliyetajwa kwa jina moja la Abdul akiwa ni mfanyabiashara kwenye magulio.
Kwa upande wake ofisa mtendaji wa kata ya Janga Michael Mwakamo alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo ilibidi mgambo wapelekwe nyumbani kwa mtuhumiwa kwa ajili ya kumchukua kwa ajili ya kutoa maelezo ni kwanini anamtesa mtoto huyo.
Mwakamo alisema kuwa mtuhumiwa huyo alichukuliwa na kwenda ofisini hapo na baada ya mahojiano ilibidi apelekwe polisi kwa hatua zaidi na baada ya mahojiano kukamilika alipelekwa Mahakama ya Mwanzo ya Mlandizi.
“Tulimuuliza ni kwani ni anamfanyia vitendo vya ukatili mtoto wake huyo wa kambo alijibu kuwa hata mumewe humpiga mtoto huyo hivyo nay eye akaona afanye hivyo lakini hakuna sababu nyingine ya yeye kumchapa kupita kiwango mtoto huyo;” alisema Mwakamo.
Hakimu wa mahakama ya Mwanzo ya Mlandizi Sharifa Mtumuya alimsomea mashitaka ya shambulio ambapo mtuhumiwa alikana shitaka hilo na kupelekwa mahabusu baada ya taratibu za dhamana kushindikana na kesi hiyo itasikilizwa tena Februari 16 mwaka huu.
Mahakama iliamuru mtoto huyo akae kwa ofisa kilimo wa kata ya Janga Neema Sonje hadi itakapoamuliwa vingine wakati kesi hiyo ikiwa inaendelea kwani haitawezekana kuendelea kukaa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi.
Mwisho.      
Na Mwandishi Wetu, Kibaha

MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewaonya baadhi ya  madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuacha mara moja tabia ya kumtishia kumfukuza kazi  Mkurugenzi  Mtendaji wa Mji huo pamoja na Mweka Hazina wake kwa madai kwamba amekataa kulipa deni la shilingi milioni 231 la mkandarasi mmoja  anayayetoa huduma mbalimbali ndani ya Halmashauri hiyo.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa mji huo mkuu huyo wa mkoa aalisema kuwa anasikitishwa na kitendo cha baadhi ya madiwani hao wa kusimamia halmashauri ili iweze kufanya kazi kwa makini na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi na  badala  yake wanafanya kazi ya kuihujumu halmashauri kwa maslahi yao binafsi.

Ndikilo alisema kuwa madiwani hao badala ya kushinikiza Halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo lakini wamekuwa wakiwapigia debe watoa huduma na kuwatisha watendaji.

“Shutuma ya baadhi ya madiwani kuhujumu halmashauri hiyo kwa kuwatishia kuwaazimia watendahi  wakuu wa mji huo kuwafukuza kazi kwa madai kwamba wamekataa  kulipa deni la shilingi milioni 231 ambazo halmashauri hiyo inadaiwa na mkandarasi mmoja anayetoa huduma ndani ya mji wa Kibaha haipendezi na wanapaswa kuangalia wajibu wao wa kuwatumikia wananchi;” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa si vema kuegemea kwa mtoa huduma wanapaswa kuacha mara moja tabia ya kuwatishia watendaji ambao wamekataa kulipa deni la mzabuni huyo
na kuacha kuingiza maslahi binafisi katika utendeji wa kazi na badala yake watimize wajibu wao wa kuisimamia halmashauri.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo Leonard Mloe alikiri kuwepo kwa taarifa za baadhi ya madiwani kutaka waungwe mkono kuweka maazimio ya kumfukuza kazi mweka hazina wa mji wa kibaha kwa kukataa kuizinisha malipo hayo.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM mkoa wa Pwani kimempongeza Rais wa awamu ya Tano Dk John Pombe Magufuli kwa kuweza kuzuia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuwabana wakwepa kodi na kuliingizia Taifa mapato yanayozidi kiasi cha trilioni tatu kwa kipindi chake cha siku 100 madarakani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu cha mkoa huo katibu mwenezi wa CCM mkoa Dk Zainab Gama akisoma tamko la mkoa kuhusu utendaji kazi wa Rais Magufuli alisema kuwa ni wa kutukuka.

Dk Gama alisema kuwa Rais ameweza kubana matumizi ya serikali na kufanikisha nchi kupata fedha nyingi ikiwa ni pamoja na kupunguza safari za nje kwa viongozi hivyo kuiwezesha serikali kubana matumizi yasiyo ya lazima ya shilingi bilioni 7 ambazo zitatumika kwenye miradi ya maendeleo.

“Jambo linguine ni kubadilisha mfumo wa sherehe za Kitaifa uliyokuwa unatumia gharama kubwa na badala yake siku za sherehe hizo ni kufanya usafi wa mazingira kote nchini;” alisema Dk Gama.

Alisema kuwa katika kuonyesha dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia wananchi aliteua baraza dogo la mawaziri ambao ni makini na hata baada ya kuteuliwa tayari wameanza kazi kwa kasi kubwa inayoendana na kauli Mbiu yake ya Hapa Kazi Tu.

“Tunaunga mkono dhamira yake ya dhati ya kuinua uchumi kuwa wa kati kwa kusisitiza kujenga viwanda na pia kuboresha mtandao wa barabara za juu katika Jiji la Dar es Salaam Fly Overs pamoja na barabara za njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze,” alisema Dk Gama.

Aidha alisema kuwa katika kipindi hicho aliweza kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watendaji wabovu katika taasisi mbalimbali za serikali ambazo walisababisha wananchi kuichukia serikali yao/
Awali akifungua kikao hicho mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao alisema kuwa katika uchaguzi ujao wa Chama utakaofanyika mwakani viongozi wanaoteua wagombea wanapaaswa kuwa makini ili kupata viongozi bora.

Mlao alisema kuwa viongozi wanaoteuliwa kukisimamia chama wanapaswa kuwa na uwezo na si mradi tu ambao baadaye wanakuja kufanya chama kinapata wakati mgumu wakati wa uchaguzi mkuu.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment