Tuesday, February 16, 2016

WAUZA MAJI WANAWAKE KWENYE MAGARI WAILILIA HALMASHAURI KUVUNJA VIBANDA VYAO

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA wanawake  wanaouza Maji ya kunywa kwenye magari  ilipokuwa mizani ya zamani ya Maili Moja wilayani Kibaha wameilalamikia Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa kuwavunjia vibanda vyao kwa madai kuwa ni uchafu licha ya kuwa wanakusanya ushuru kwao.
Moja ya wafanyabiashara hao ambao ni Veronica Damiani akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa wanashangaa Halmashauri hiyo kuwavunjia vibanda vyao bila ya kuwaandikia barua ya kuwataka wasifanye biashara zao.
Damiani alisema kuwa wao wanajua serikali kabla ya kufanya kitu lazima itoe taarifa ya maandishi kabla ya kufanya jambo lolote lakini wao wanashangaa kuondolewa bila ya kupewa barua ya kuwahamisha katika eneo hilo.
“Sisi hatukatai kuondoka ila wangetupa taarifa juu ya kututaka tuondoke katika eneo hili na siku chache zilizopita walikuja wakatuambia kuwa tuendelee na biashara wakati majadiliano yanaendelea lakini tunashangaa jana wamekuja na migambo na kutubomolea vibanda vyetu huku wakitupa masaa matatu kwa ajili ya kuhama,” alisema Damiani.
Alisema kuwa sasa wao watenda wapi kufanya biashara kwani maji wanayouza wengine wamekopa mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa lengo la kujipatia kipato chao na familia zao ambapo wengine ni wajane.
“Tunakopa fedha kwa ajili ya kufanyabiashara hizi sasa tutarejeshaje fedha tulizokopa tunaomba viongozi wa ngazi za juu watuangalie kwa jicho la huruma hatuna kipato kingine zaidi ya biashara hizi ambazo zinatusaidia kuwasomesha watoto wetu kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo,” alisema Damiani.
Kwa upande wake Mhandisi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Dismas Marango akijibu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Gladys Dyamvunye alisema kuwa wafanyabiashara hao walikuwa wakifanyabiashara zao kimakosa kwani hawakuwa na kibali chakufanyia biashara kwenye eneo hilo.
Marango alisema kuwa hawakuwapa barua kwani sehemu hiyo si kwa ajili ya kufanyabiashara na kwamba mabanda hayo yanaonekana kama uchafu na waliwapa taarifa kwa maneno wiki tatu zilizopita za kuwataka waondoke kwenye eneo hilo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment