Na John Gagarini, Kibaha
WATU 53,446 wilayani Rufiji mkoani Pwani wamekumbwa na mafuriko hali iliyowafanya wazungukwe na
maji na kuhitaji msaada kufuatia mvua za Vuli zinazoendelea hapa nchini.
Aidha tayari boti mbili za uokozi tayari zimepelekwa kwenye
maeneo hayo kwa ajili ya kuwaondoa watu hao waliozungukwa na maji na kuwapeleka
sehemu salama.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu toka
kwenye eneo la tukio, Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema
kuwa maji hayo ambayo yametoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkoa wa
Morogoro.
“Vijiji vingi wilayani humo vimezingirwa na maji na watu
wengi waliokumbwa na kadhia hiyo ni wale waliohamia mashambani kwa ajili ya
kilimo na kukutwa na maji hayo pamoja na nyumba ambazo ziko mabondeni,” alisema
Ndikilo.
Alisema kuwa mvua hizo ambazo zilizoanza kidogo kidogo tangu Januari
31 mwaka huu zimeathiri zaidi kwenye maeneo ya kata za Mwaseni, Tarafa ya
Mkongo, Tarafa ya Ikwiriri na kata ya Muhoro.
“Kutokana na athari za mvua hizo hekta zaidi ya 7,000 za Mahindi
na hekta zaidi ya 8,000 za Mpunga zimesombwa
na maji na tayari mkoa umewasiliana na Waziri Mkuu kwenye kitengo cha Wakala wa
mazao kuomba msaada wa chakula tani 1,280 za mahindi,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa wameteua wafanyabiashara sita kwa ajili ya
kununua mahindi na kuyasaga kwa ajili ya chakula ikiwa ni njia ya kuwasaidia
wananchi pia kukabili mfumuko wa bei ambao unaweza kujitokeza kutokana na hali
hiyo.
Katika hatua nyingine mkoa umeomba tani 10 za mbegu za
mahindi na tani tano za mbegu za Mtama kwa ajili ya kupanda kukabiliana na
athari ya mazao ambayo yamesombwa na maji ya mvua za Vuli ambazo wiki ijayo
zitaanza mvua za Masika.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI imeombwa kuipatia Idara ya Ziamamoto mkoani Pwani
vifaa kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya moto na kuokoa watu wanaokumbwa na
majanga mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini
Kibaha Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto mkoani Pwani Goodluck Zelote alisema kuwa
kutokana na uhaba wa vifaa baadhi ya wilaya hazina vituo vya zimamoto.
Zelote alisema kuwa kwenye mkoa wa Pwani kati ya wilaya sita
ni wilaya tatu tu za Kibaha, Bagamoyo na Mafia ndiyo zenye vikosi hivyo huku
wilaya za Kisarawe, Rufiji na Mkuranga zikiwa hazina huduma hiyo.
“Ingependeza angalau kila wilaya kuwa japo na kikosi cha Zimamoto
na uokoaji japo hakitaweza kutoa huduma kwenye eneo lote lakini angalau
zingesaidia ambapo kwa sasa utendaji kazi unakuwa mgumu,” alisema Zelote.
Alisema kuwa vifaa hivyo ni magari pamoja na vifaa vya
uokoaji ambapo alitoa mfano wa ajali ya moto ambayo ilitokea hivi karibuni
Chalinze walifika na kunusuru nyumba yote kuteketea kwa moto lakini kutokana na
umbali uliopo walinusuru vyumba kadhaa.
“Kwa sasa tunachokifanya ni kutoa elimu zaidi ya kujikinga na
kuzuia moto kwa kutumia vifaa vya kuzimia moto ambavyo kila mtu anapaswa kuwa
navyo kuanzia kwenye maeneo ya huduma hadi majumbani,” alisema Zelote.
Aidha alisema kuwa moja ya changamoto wanayoipata ni ujenzi
holela ambao hauzingatii mipango miji hali ambayo inasababisha magari ya
kuzimia moto kushindwa kufika kwenye nyumba ambazo zinawaka moto na kuwataka
watu wazingatie kanuni za ujenzi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment