Tuesday, February 16, 2016

MADEREVA BODABODA KUWA NA UTAMBULISHO

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki wilayani Kibaha mkoani Pwani (CHAWAMAPIKI) kimeandaa utaratibu wa kuwa na makoti maalumu ambayo yanayongaa ambayo yatakuwa na namba mgongoni ili kukabiliana na madereva wanaokiuka taratibu za uendeshaji pikipiki.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa chama hicho Hussein Kijazi alisema kuwa kumekuwa na lawama nyingi kwa madereva wa Bodaboda kukiuka taratibu za uendeshaji hali ambayo inaweza kuchangia kuongezeka kwa ajali.
Kijazi alisema kuwa ili kuwadhibiti madereva wanaokiuka taratibu wameona bora waanzishe utaratibu huo ili iwe rahisi kuwabaini wale wanokwenda kinyume cha sheria na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Utaratibu huu tunatarajia utaanza wakati wowote kuanzia sasa kwani kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa watu mbalimbali wakilalamika kuwa madereva hao wanavunja sheria na kuwa moja ya chanzo cha ajali,” alisema Kijazi.
Alisema kuwa mtu akiona kuna tataizo kwa dereva fulani anataja tu namba na wao watafuatilia ni dereva gani mwenye hiyo namba kisha chama kitamwita na kumpa adhabu inayostahili kutokana na kosa lake.
“Makoti hayo yanayongaa hata nyakati za usiku yatatusaidia kuwabaini madereva wanaokiuka utartibu wetu ambao tumejiwekea kwani baadhi ya watu wanalalamika kuwa madereva wengine wanajihusisha na vitendo vya uhalifu lakini wakiwa na makoti hayo itakuwa ni vigumu kuvunja taratibu kwani lazima watajulikana na wataadhibiwa,” alisema Kijazi.
Aidha wameipongeza serikali kwa kufuta baadhi ya kodi zikiwemo zile za TRA 90,000, Motor Vehicle 50,000 na kodi ambazo zilikuwa ni kero kwao. Chama hicho kinawanachama 400 na wamiliki zaidi ya 100 na wana vituo 13 na kina lengo la kusaidia wakati wa matatizo ikiwa ni pamoja na kufiwa.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment