Thursday, February 25, 2016

BIBI AINGIA MATATANI KIFO CHA MWANAE

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
BIBI Nuru Mchenga mwenye umri wa zaidi ya miaka (80) mkazi wa Maili Moja B wilayani Kibaha mkoani Pwani amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya wananchi kumlalamikia kukaa na maiti ya mwanae kwa masaa kadhaa bila ya kuwataarifu watu.
Mbali ya kumshangaa kukaa na maiti muda mrefu pia walimshangaa bibi huyo kumsafisha mwanae kwa taratibu za dini ya Kiislamu jambo ambalo ni kinyume kwani huwa linafanywa na wanaume.
Tukio hilo lilitokea Fabruari 24 majira ya mchana ambapo Mwanae Kassimu alifariki majira ya saa nane hapo nyumbani kwake baada ya kudaiwa kuwa alikuwa anaumwa.
Wakizungumza na waandishi wa habari majirani wa Bibi huyo ambao hawakutaka kutajwa majina yao magazetini walisema kuwa wameshangazwa na kitendo hicho cha kukaa na maiti kwa muda wote huo bila kuomboleza kama ilivyo kwa watu wanaofiwa ambao hulio kuashiria kuwa kuna msiba.
Walisema kuwa kilichowashangaza ni jinsi gani bibi huyo alipomfanyia usafi mwanae wa kiume jambo ambalo ni kinyume na taratibu za dini ya Kiislamu hali ambayo ndiyo imezua maswali mengi.
Alisema marehemu alipaswa kufanyiwa taratibu za kidini na mwanaume na si mwanamke kama alivyofanya bibi huyo ambaye watu wengi wamemshangaa kwa ujasiri huo.
“Inasikitisha sana kuona bibi huyu anafanya vitu kama hivyo ndiyo maana kumekuwa na maneno mengi kutokana na kifo cha mwanae kutokana na alivyofanya na pia haonyeshi kusikitika kifo cha mwanae tofauti na misiba mingine,”  walisema majirani hao.
Kwa upande wake Bibi huyo akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake alisema kuwa mwanae alilogwa kwa kutupiwa jini na watu ambao hawaipendi familia yake na kusababisha kifo hicho.
Mchenga alisema kuwa siku ya tukio hilo mwanae alikuwa tu nyumbani nay eye alikuwa akiendelea na shughuli zake na kushangaa kuona mwanae hana uchangamfu.
“Ilipofika mchana mwanangu alifariki na kabla hajafariki tulikubaliana nikifa mimi yeye ataniosha na akifa yeye mimi nitamwosha ndiyo sababu ya mimi kufanya hivyo,” alisema Mchenga.
Alisema kuwa anashangaa kuona watu wanataka kumfanyia fujo nyumbani kwake na kusema kuwa watu wanasema maneno mengi juu ya kifo cha mwanae huyo.
Kutokana na watu kujazana nyumbani kwa bibi huyo ilibidi jeshi la polisi kuuchukua mwili wa marehemu majira ya saa 3 usiku na baadaye walirudi tena majira ya saa tano kasoro na kumchukua bibi huyo kutokana na kuhofia usalama wake kwani watu walikuwa wakimzonga na kumzomea, Jeshi la polisi limethibitisha kutokea tukio hilo.
Mwisho.
  



No comments:

Post a Comment