Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Nchini (NFRA) imeupatia mkoa wa pwani tani 1,283 za mahindi kwa ajili ya wahanga wa mafuriko wilayani Rufiji.
Mahindi hayo yatasagwa kwa ajili ya kuwapatia unga bure wananchi 53,446 kwenye tarafa za Mkongo,Ikwiriri na muhoro wilayani humo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini kibaha mkuu wa mkoa wa pwani injinia evarist ndikilo alisema kuwa mahindi hayo yaliwasili juzi wilayani humo.
"Tunatarajia mahindi hayo yatawawasaidia waathirika hao, kisha yatasagwa na wananchi walioathirika watapewa bure," alisema ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa tayari magari ya kubeba mahindi hayo kutoka halmashauri yameshachukua mahindi hayo ya msaada kwa kipindi cha mwezi Februari na Machi
" Pia tumeteua wafanyabiashara sita ambao watanunua mahindi kwa wakala hao kisha kuyauza kwa bei ndogo ili kila mwananchi amudu kununua," alisema ndikilo.
Aidha alisema mkakati uliopo kwa sasa wa kiwasaidia wananchi hao ni kuhamasisha wafanyabiashara kupeleka bidhaa kama Michele,unga na maharage, kufanya tathmini ya mafuriko, kuhamasisha kulima mazao ya muda mfupi Mtama, viazi, kunde na muhogo.
"Hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya kifo kilichotokana na mafuriko hayo ambayo yameathiri watu ambao wanalima kandokando ya Mto rufiji ambapo Daraja la mto muhoro limefunikwa na maji," alisema ndikilo.
Aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kutoa misaada ya kiutu kwa waathirika wa mafuriko hayo yaliyoathiri hekta 8,133 za mpunga na hekta 7,171 za Mahindi.
Chanzo cha mafuriko hayo yalianza kuingia kijiji cha mloka tarehe 31 januari hadi februari 6 ambapo maji hayo yametokea mto rufiji unaopokea maji ya mvua kutoka mikoa Iringa, Mbeya na Morogoro.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment