Thursday, February 25, 2016

ACHOMWA MOTO KWA WIZI WA MCHELE DUKANI

Na John Gagarini, Kibaha
MTU mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Ngozi mkazi wa Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani ameuwawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali kwa madai ya kuiba mchele na mafuta ya kupikia dukani.
Tukio hilo lilitokea Fabruari 25 majira ya saa 9 alfajiri katika mtaa wa Tangini baada ya marehemu akiwa na mwenzake ambaye alikimbia kuvunja na kutoa mchele huo kilogramu 100 na mafuta ya lita tatu galoni mbili.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa huo Leons Karoli alisema kuwa watu hao waligunduliwa na baadhi ya madereva wa Bodaboda waliokuwa wakipita kwenye eneo la tukio na kuwakuta watuhumiwa hao wakiwa na vitu hivyo wakiwa wamevipakia kwenye pikipiki ya marehemu aina ya Boxer.
“Mashuhuda walisema kuwa marehemu alikuwa ndani ya hilo duka na kujifanya kama ndiye mwenye duka akijifanya ndiyo analifungua lakini watu walikuwa na wasiwasi kwani ilikuwa ni asubuhi sana jambo ambalo si la kawaida kwa mmiliki huyo kulifungua muda huo huku ambaye mmiliki wake ni Mmbando,” alisema Karoli.
Karoli alisema kuwa baada ya watu kuwa na wasiwasi waliwasiliana na watu kujaa kisha kuanza kumpiga marehemu hadi alipopoteza fahamu na mwenzake alifanikiwa kutoroka kwa kukimbia na kumwacha mwenzake ambaye alibainika kuwa ni muuza matunda pia ni dereva bodaboda.
“Tulifanya mawasiliano na polisi na kuwajulisha kuwa kuna mwizi kakamatwa lakini kabla hawajafika watu hao wenye hasira walimpiga kisha kumchoma moto kwa kutumia mafuta ya petroli na kusababisha kifo chake,” alisema Karoli.
Alisema kuwa marehemu alikuwa na begi ambalo lilikuwa na vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkasi mkubwa unaotumika kukatia makufuli, nondo, vocha za simu pamoja na fedha taslimu kiasi cha shilingi 150,000.
Jeshi la polisi mkoani Pwani lilithibitisha kutokea tukio hilo na kuwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi kwa kutoa taarifa polisi kwa hatua zaidi za kisheria na si kuwauwa watuhumiwa wa matukio ya kihalifu.
Mwisho.
  



No comments:

Post a Comment