Tuesday, February 16, 2016

KATA KUKUTANA NA WAKULIMA NA WAFUGAJI

Na John Gagarini, Pwani
KATA ya Kiwangwa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani imeweka mpango wa kukutana na wakulima na wafugaji ili kukabiliana na changamoto za jamii hizo ambazo zimekuwa zikigombana kutokana na wafugaji kudaiwa kulisha mazao mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu diwani wa kata hiyo Hussein Malota alisema kuwa lengo la kukutana na pande hizo ni kujadili jinsi gani ya kukabili changamoto hizo ambazo zimekuwa zikisababisha mapigano.
Malota alisema kuwa wiki tatu zilizopita kulitokea ugomvi baina ya pande hizo mbali baada ya wafugaji kudaiwa kuachia ngombe na kula mazao ya wakulima hali ambayo ili sababisha vurugu za hapa na pale.
“Tayari tumeunda kamati za maridhiano za wakulima watano na wafugaji watano ili kutunga sheria ndogondogo ambazo endapo mmoja atakiuka ataadhibiwa kulingana na makubaliano ya kamati hiyo ili kudhibiti wale watakaokiuka makubaliano hayo,” alisema Malota.
Alisema kuwa tatizo kubwa ni baadhi ya wafugaji wapya wanaoingia kwenye vijiji mbalimbali kwani hawajui taratibu mara waingiapo kwenye maeneo ya wenyeji hali ambayo inasababisha migogoro baina ya pande hizo.
“Tumeunda kamati hizi ili zitunge sheria ambazo zitawaabana wale watakaokiuka kwani wajumbe wa hizo kamati watawajulisha wenzao makubaliano yaliyoafikiwa lengo likiwa ni kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji waishi kwa amani kama jamii moja,” alisema Malota.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine walioiona ni baadhi ya wafugaji kuwaachia watoto wachunge mifugo hiyo ambayo ni makundi makubwa na kushindwa kuyamudu wakati wakichunga na kusababisha matatizo.
Mwisho.

          

No comments:

Post a Comment