Na John Gagarini, Kibaha
SHEILA Husein mkazi wa Janga Kata ya Janga Mlandizi wilayani
Kibaha mkoani Pwani amejikuta matatani baada ya kumpiga mtoto wake wa kambo wa
kiume mwenye umri wa miaka (2) na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili ikiwa ni
pamoja na kumvuta sehemu zake za siri.
Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa Mtaa wa
Janga na Diwani wa kata hiyo Chande Mwalika alisema kuwa mtoto huyo amekuwa
akipigwa kila siku kwa fimbo hali ambayo imemfanya awe na makovu mengi mwilini.
Mwalika alisema kuwa moja ya majirani ambaye alishindwa
kuvumilia vitendo hivyo Adinani Mkupa nakutoa taarifa hiyo alisema kuwa vitendo
vilivyokuwa vikifanywa na mtuhumiwa huyo ni vya kikatili na haviwezi
kuvumilika.
“Amekuwa akimchapa mwanae kwa fimbo bila ya kumuonea huruma
hali ambayo imemfanya mtoto huyo aharibike mwili mzima kutokana na vipigo hivyo
na kibaya zaidi ni pale alipofikia hatua ya kumvuta sehemu zake za siri na
hakuna sababu maalumu inayomfanya amwazibu mtoto huyo kwani bado ni mdogo sana
na hana uwezo wa kuongea,” alisema Mwalika.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo ilibidi watoe ripoti kwa
kwenye uongozi wa kata kwa ajili ya hatua zaidi kwa mtuhumiwa ambaye ni mama wa
nyumbani huku mumewe aliyetajwa kwa jina moja la Abdul akiwa ni mfanyabiashara
kwenye magulio.
Kwa upande wake ofisa mtendaji wa kata ya Janga Michael
Mwakamo alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo ilibidi mgambo wapelekwe
nyumbani kwa mtuhumiwa kwa ajili ya kumchukua kwa ajili ya kutoa maelezo ni
kwanini anamtesa mtoto huyo.
Mwakamo alisema kuwa mtuhumiwa huyo alichukuliwa na kwenda
ofisini hapo na baada ya mahojiano ilibidi apelekwe polisi kwa hatua zaidi na
baada ya mahojiano kukamilika alipelekwa Mahakama ya Mwanzo ya Mlandizi.
“Tulimuuliza ni kwani ni anamfanyia vitendo vya ukatili
mtoto wake huyo wa kambo alijibu kuwa hata mumewe humpiga mtoto huyo hivyo nay
eye akaona afanye hivyo lakini hakuna sababu nyingine ya yeye kumchapa kupita
kiwango mtoto huyo;” alisema Mwakamo.
Hakimu wa mahakama ya Mwanzo ya Mlandizi Sharifa Mtumuya
alimsomea mashitaka ya shambulio ambapo mtuhumiwa alikana shitaka hilo na
kupelekwa mahabusu baada ya taratibu za dhamana kushindikana na kesi hiyo
itasikilizwa tena Februari 16 mwaka huu.
Mahakama iliamuru mtoto huyo akae kwa ofisa kilimo wa kata
ya Janga Neema Sonje hadi itakapoamuliwa vingine wakati kesi hiyo ikiwa
inaendelea kwani haitawezekana kuendelea kukaa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo
amewaonya baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuacha mara
moja tabia ya kumtishia kumfukuza kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Mji
huo pamoja na Mweka Hazina wake kwa madai kwamba amekataa kulipa deni la
shilingi milioni 231 la mkandarasi mmoja anayayetoa huduma mbalimbali
ndani ya Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao cha baraza la
madiwani wa mji huo mkuu huyo wa mkoa aalisema kuwa anasikitishwa na kitendo
cha baadhi ya madiwani hao wa kusimamia halmashauri ili iweze kufanya kazi kwa
makini na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi na badala yake
wanafanya kazi ya kuihujumu halmashauri kwa maslahi yao binafsi.
Ndikilo alisema kuwa madiwani hao badala ya
kushinikiza Halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo lakini wamekuwa wakiwapigia
debe watoa huduma na kuwatisha watendaji.
“Shutuma ya baadhi ya madiwani kuhujumu
halmashauri hiyo kwa kuwatishia kuwaazimia watendahi wakuu wa mji huo
kuwafukuza kazi kwa madai kwamba wamekataa kulipa deni la shilingi
milioni 231 ambazo halmashauri hiyo inadaiwa na mkandarasi mmoja anayetoa
huduma ndani ya mji wa Kibaha haipendezi na wanapaswa kuangalia wajibu wao wa
kuwatumikia wananchi;” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa si vema kuegemea kwa mtoa huduma
wanapaswa kuacha mara moja tabia ya kuwatishia watendaji ambao wamekataa kulipa
deni la mzabuni huyo
na kuacha kuingiza maslahi binafisi katika
utendeji wa kazi na badala yake watimize wajibu wao wa kuisimamia halmashauri.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya
mji huo Leonard Mloe alikiri kuwepo kwa taarifa za baadhi ya madiwani kutaka
waungwe mkono kuweka maazimio ya kumfukuza kazi mweka hazina wa mji wa kibaha
kwa kukataa kuizinisha malipo hayo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM mkoa wa Pwani
kimempongeza Rais wa awamu ya Tano Dk John Pombe Magufuli kwa kuweza kuzuia
mianya ya upotevu wa mapato kwa kuwabana wakwepa kodi na kuliingizia Taifa
mapato yanayozidi kiasi cha trilioni tatu kwa kipindi chake cha siku 100
madarakani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini
Kibaha wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu cha mkoa huo katibu mwenezi wa CCM
mkoa Dk Zainab Gama akisoma tamko la mkoa kuhusu utendaji kazi wa Rais Magufuli
alisema kuwa ni wa kutukuka.
Dk Gama alisema kuwa Rais ameweza kubana
matumizi ya serikali na kufanikisha nchi kupata fedha nyingi ikiwa ni pamoja na
kupunguza safari za nje kwa viongozi hivyo kuiwezesha serikali kubana matumizi
yasiyo ya lazima ya shilingi bilioni 7 ambazo zitatumika kwenye miradi ya
maendeleo.
“Jambo linguine ni kubadilisha mfumo wa
sherehe za Kitaifa uliyokuwa unatumia gharama kubwa na badala yake siku za
sherehe hizo ni kufanya usafi wa mazingira kote nchini;” alisema Dk Gama.
Alisema kuwa katika kuonyesha dhamira yake ya
dhati ya kuwatumikia wananchi aliteua baraza dogo la mawaziri ambao ni makini
na hata baada ya kuteuliwa tayari wameanza kazi kwa kasi kubwa inayoendana na kauli
Mbiu yake ya Hapa Kazi Tu.
“Tunaunga mkono dhamira yake ya dhati ya
kuinua uchumi kuwa wa kati kwa kusisitiza kujenga viwanda na pia kuboresha
mtandao wa barabara za juu katika Jiji la Dar es Salaam Fly Overs pamoja na barabara
za njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze,” alisema Dk Gama.
Aidha alisema kuwa katika kipindi hicho
aliweza kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watendaji wabovu katika taasisi
mbalimbali za serikali ambazo walisababisha wananchi kuichukia serikali yao/
Awali akifungua kikao hicho mwenyekiti wa CCM
mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao alisema kuwa katika uchaguzi ujao wa Chama utakaofanyika
mwakani viongozi wanaoteua wagombea wanapaaswa kuwa makini ili kupata viongozi
bora.
Mlao alisema kuwa viongozi wanaoteuliwa
kukisimamia chama wanapaswa kuwa na uwezo na si mradi tu ambao baadaye wanakuja
kufanya chama kinapata wakati mgumu wakati wa uchaguzi mkuu.
Mwisho.