Na John Gagarini,
Kibaha
WAKAZI wa Mitaa ya Vikawe,
Vikawe Shuleni, Vikawe Bondeni na Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wamepatiwa
ofa ya kutumia maji bure kwa miezi mitatu baada ya huduma hiyo kuanza
kupatikana ambapo mitaa hiyo haikuwa na maji ya bomba tangu kuanzishwa kwake.
Maji hayo tayari
yameshaanza kutoka yanatokana na chanzo cha maji cha Ruvu Juu baada ya mitaa
hiyo kutokuwa na maji kabisa ambapo awali walikuwa wakitumia maji ya visima na
mto .
Akizungumza na
mabalozi, makatibu na viongozi wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya
Mkuza wilayani Kibaha wakati wa semina ya viongozi hao iliyofanyika jana mjini
Kibaha, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Silvestry Koka alisema kuwa maji yameanza
kutoka kwenye mitaa hiyo hivi karibuni.
“Wananchi hao wamepata
ofa hiyo ya kutumia maji bure lakini baada ya miezi mitatu wataanza kuyalipia
maji hayo baada ya kukosa maji ya bomba kwani kulikuwa hakuna maji kabisa na
walikuwa wakichota maji kwenye visima na mto ambapo baadhi walipoteza maisha
kwa kukamatwa na mamba walipokuwa wakichota maji mtoni,” alisema Koka.
Katika hatua nyingine
Koka alisema kuwa mji wa Kibaha utaondokana na tatizo kubwa la ukosefu wa maji
baada ya mradi wa bomba kubwa kutoka chanzo cha mto Ruvu kuanza.
Koka alisema kuwa kwa muda
mrefu wa mji huo umekuwa ukikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji
huku wakati mwingine maji yakiwa yanatoka kwa mgao kutokana na chanzo kilichopo
kutokuwa na uwezo wa kutoa maji ya kutosha.
“Mradi huu kwa sasa
uko kwenye hatua nzuri ambapo uchimbaji wa mtaro utaanza muda wowote kuanzia
sasa kwani taratibu zingine zimekamilika na bomba litakalopitishwa litakuwa ni
kubwa ambalo litapitisha maji mengi,” alisema Koka.
Kwa upande wake katibu
wa (CCM) Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni utekelezaji
wa ilani ya chama ambayo ni ahadi kwa
wananchi ili kuboresha utoaji huduma.
Mdimu alisema kuwa
chama kupitia kwa viongozi wake kitahakikisha ahadi zote zinatekelezwa kwa
wakati uliopangwa ili wananchi waondokane na kero za huduma muhimu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment