Sunday, July 27, 2014

MEYA AWATAKA WAISLAMU KUDUMIASHA AMANI NA UPENDO IDDI



Na John Gagarini, Bagamoyo
WAISLAMU kote nchini wametakiwa kusherehekea sikuu ya Eid el Fitr kwa upendo na amani ili funga yao ya mwezi mzima iwe na maana na kuacha kufanya vitendo viovu ambavyo ni kinyume na mapenzi ya Mungu.
Ushauri huo umetolewa jana mjini Bagamoyo na meya wa Mji wa huo Abdul Sharifu, wakati alipokuwa akifuturisha watu wenye mahitaji maalumu na waumini wa dini hiyo kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Sharifu alisema kuwa funga hiyo itakuwa na maana endapo waislamu wataisherehekea kwa kuzingatia imani ya dini ya kiislamu na si kinyume na dini inavyosema.
“Baadhi ya waislamu wamekuwa wakiitumia siku hiyo kwa ajili ya kufanya matendo ambayo hayampendezi mwenyezi Mungu hali ambayo inafanya waonekane mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa hawakufunga kutokana na kwenda kinyume na imani inavyosema,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa pia watumie siku hiyo kwa ajili ya kujitolea kuwasaidia  watu wenye mahitaji maalumu kama vile watu wenye ulemavu, yatima, wajane na wagonjwa na watu wenye shida mbalimbali ili iwe sadaka ambayo itampendeza Mungu.
Sharifu ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo aliwataka waumini wa dini hiyo na wale wasio wa imani hiyo kuitumia siku hiyo kwa ajili ya kumtafakari mwenyezi Mungu.
 Wakati huo huo wenye uwezo mkoani Pwani wametakiwa kumtukuza Mungu katika kipindi cha siku kuu ya Eid el Fitr kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji ili wapate thawabu mbele ya mwenyezi Mungu.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Mkoani Pwani, Method Mselewa  ambaye alimwakilisha mbunge huyo Silvestry Koka wakati wa kutoa mkono wa Iddi kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutoka misikiti mbalimbali wilayani hapa.
Mselewa alisema kuwa kutoa wakati wa kipindi hichi ni sadaka ambayo ina manufaa makubwa kwa waislamu hivyo wawe na moyo wa kuwasaidia watu wenye uhitaji ili nao wajisikie kama kuna watu wanawajali.
“Mbunge kila mwaka kipindi kama hichi amekuwa akijitolea kwa makundi hayo ambayo ni pamoja na wazee, yatima, wajane na wale wasiojiweza ambapo kila msikiti wanatoka watu 20 ili nao waweze kuandaa futari kwa familia zao,” alisema Mselewa.
Alisema kuwa waumini hao wanatoka kwenye misikiti 64 iliyopo katika Jimbo la Kibaha ambapo kila mmoja anapewa mkono wa Iddi ambao ni mchele kilogramu mbili, sukari kilogramu moja na fedha kwa ajili ya kununulia mboga.
Aidha alisema kuwa mbali ya kuwapatia vitu hivyo pia huwapatia ujumbe wa Iddi wa kudumisha amani, upendo na ushirikiano kwa watu wote katika kipindi hichi na nyakati zingine ambazo si za mfungo.
Alibainisha kuwa mbali ya makundi hayo pia mkono wa Iddi unatolewa kwa viongozi wa chama wakiwemo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Baraza la Wanawake (UWT), Baraza la Wazazi na Umoja wa Vijana (UVCCM) ambapo jumla ya watu 2,000 watafikiwa.
Mwisho.
     

No comments:

Post a Comment