Na John Gagarini, Kibaha
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatarajia kujenga
kituo kikubwa cha kutunza kumbukumbu za shughuli za mamlaka hiyo ambacho
kitakuwa ni cha kipekee kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kituo hicho kitajengwa eneo la Halmashauri ya mji wa Kibaha
wilayani Kibaha mkoani Pwani ambapo kwa sasa tayari wamepata mjenzi na hatua za
ujenzi ziko kwenye mchakato.
Akizungumza mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa Usajili wa
watu mkoani humo, mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Dickson Maimu alisema kuwa
tayari wameshapata eneo kwa ajili ya ujenzi huo.
“Ujenzi wa kituo cha NIDA ambacho kitatunza kumbukumbu za
Watanzania wote utaanza wakati wowote ambapo tutapata msaada kutoka serikali ya
watu wa Korea,” alisema Maimu.
Maimu alisema kuwa wanaishukuru Halmashauri ya Mji wa Kibaha
na mkoa kwa kuwapatia eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na makazi ya
watumishi wa mamlaka hiyo ambapo kwa sasa wamepata ofisi za muda kwa ajili ya
kuendeshea zoezi hilo lililoanza mkoani Pwani Julai Mosi.
Katika hatua nyingine alisema kuwa zoezi hilo ambalo limeanza
litakuwa na lengo la kutambua uraia wa watu wenye umria kuanzia miaka 18 na
kuendelea kwa wananchi wanaoishi nchini na kuandikishwa taarifa zao.
Alisema kuwa mamlaka hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2008 na
kuanza zoezi hilo kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar litajenga utawala
bora wa mamlaka ya kutunza daftari la taifa la utambuzi na usajili wa watu kwa
kushirikiana na wadau walioteuliwa.
“Mfumo wa Taifa wa utambuzi umeleta mabadiliko na usajili wa
watu umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika serikali nyingi
duniani zinazotumia mfumo huu,” alisema Maimu.
Mkurugenzi huyo wa NIDA alisema kuwa mamlaka itatoa
vitambulisho vya makundi matatu ya Watanzania, wageni wakaazi na wakimbizi
ambapo katika kudhibiti waombaji ambao si raia wanaoomba vitambulisho
vimeshirikishwa vyombo vya dola ikiwa ni pamoja na kamati za ulinzi na usalama
za mitaa, idara ya uhamiaji, polisi na usalama wa Taifa wanaopitisha maombi ili
kuwaengua wasio raia.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment