Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani
Pwani limewataka madereva kuwa makini waendeshapo magari na kuacha matumizi ya
vilevi ili kuepukana na ajalizisizo za lazima ambazo zinaweza zikajitokeza
wakati wa kipindi cha sikukuu ya Eid el Fitr inayofanyika leo duniani kote.
Pia limewataka wanafamilia
kutotoka wote majumbani bila ya kuacha watu au kutoa taarifa kwa majirani ili
kuepuka wizi na uhalifu unaoweza kujitokeza wakati wa sikukuu.
Kwa mujibu wa kamanda wa
polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP)
Ulrich Matei alisema kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakitumia vilevi wakati
wa kiendesha magari jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri
na watembea kwa miguu.
“Jeshi la polisi liko
makini katika kipindi hichi cha sikukuu ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea
sikukuu bila ya matatizo na linawaomba madereva kuachana na tabia ya kutumia
vilevi ili kuepuka ajali wakati huu,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alisema kuwa kikosi
cha usalama barabarani kitahakikisha madereva wanafuata sheria za usalama
barabarani ili kuepusha ajali ambazo zianweza kutokea na kuleta madhara kwa
watu.
“Tunasisitiza madereva
kuachana na ulevi wakati wa kuendesha kwani uzoefu unaonyesha ajali nyingi
zimekuwa zikitokana na matumizi ya ulevi hivyo waache matumizi hayo na endapo
watabainika watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Kamanda Matei.
Kwa upande wa wananchi
aliwataka kutumia ulinzi jirani kwa kuacha mtu au watu badala ya kuondoka wote
na kuacha nyumba peke yake jambo ambalo linaweza likasababisha wizi majumbani.
“Wezi wamekuwa wakitumia
mwanya wa kuiba kwenye nyumba ambazo hazina watu hivyo hata kama nyumba nzima
imetoka ni vyema wakatoa taarifa kwa majirani ili wawalindie nyumba zao,”
alisema Kamanda Matei.
Aliwataka wamiliki wa kumbi
za starehe kutojaza watu kupita kiasi ili kuepuka athari ambazo zinaweza
kujitokeza endepo watakuwa wamejaza watu wengi kwenye kumbi zao.
“Kuna hatari nyingi
zinazotokana na kumbi kujaa kupita kiasi mfano watu kukosa hewa na kusababisha
vifo au bahati mbaya shoti ya umeme endapo itatokea hivyo lazima wazingatie
masharti ya leseni zao zinavyowataka ili kuepusha athari kama hizo,” alisema
Kamanda Matei.
Alibainisha kuwa jeshi lake
limejipanga kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinafanyika kwa amani na utulivu kwa
kuweka ulinzi kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya doria
mitaani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment