Saturday, July 26, 2014

WENYE UWEZO WAWASAIDIE WENYE MAHITAJI



Na John Gagarini, Kibaha
WATU wenye uwezo mkoani Pwani wametakiwa kumtukuza Mungu katika kipindi hichi cha mfungo mtukufu wa Ramadhan kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji ili wapate thawabu.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Mkoani Pwani, Method Mselewa  ambaye alimwakilisha mbunge huyo Silvestry Koka wakati wa kutoa mkono wa Iddi kwa waumini wa dini ya Kiislamu kutoka misikiti mbalimbali wilayani hapa.
Mselewa alisema kuwa kutoa wakati wa kipindi hichi ni sadaka ambayo ina manufaa makubwa kwa waislamu hivyo wawe na moyo wa kuwasaidia watu wenye uhitaji ili nao wajisikie kama kuna watu wanawajali.
“Mbunge kila mwaka kipindi kama hichi amekuwa akijitolea kwa makundi hayo ambayo ni pamoja na wazee, yatima, wajane na wale wasiojiweza ambapo kila msikiti wanatoka watu 20 ili nao waweze kuandaa futari kwa familia zao,” alisema Mselewa.
Alisema kuwa waumini hao wanatoka kwenye misikiti 64 iliyopo katika Jimbo la Kibaha ambapo kila mmoja anapewa mkono wa Iddi ambao ni mchele kilogramu mbili, sukari kilogramu moja na fedha kwa ajili ya kununulia mboga.
“Watu wamekuwa wakifuturisha kwa kuwalisha watu chakula lakini Mbunge kaamua kubadili staili kwa kuwapa vyakula hivyo ambapo wao watenda kuziandalia familia zao tofauti na kuwapa chakula ambapo watakaokula ni wachache tofauti na watakapopeleka nyumbani kuandaa wenyewe kwani yeye hawezi kuja na familia balia atakuja mtu mmoja,” alisema Mselewa.
Aidha alisema kuwa mbali ya kuwapatia vitu hivyo pia huwapatia ujumbe wa Iddi wa kudumisha amani, upendo na ushirikiano kwa watu wote katika kipindi hichi na nyakati zingine ambazo si za mfungo.
Alibainisha kuwa mbali ya makundi hayo pia mkono wa Iddi unatolewa kwa viongozi wa chama wakiwemo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya, Baraza la Wanawake (UWT), Baraza la Wazazi na Umoja wa Vijana (UVCCM) ambapo jumla ya watu 2,000 watafikiwa.
Mwisho.
     

No comments:

Post a Comment