Na John Gagarini, Kibaha
KIJANA aliyetambuliwa kwa jina la Omary Iddi mkazi wa Kijiji
cha Mwanabwito kata ya Ruvu wilayani Kibaha mkoani Pwani anayekadiriwa kuwa na
umri wa miaka (25) anatuhumiwa kumwua mkewe kwa kumchoma kisu kutokana na wivu
wa mapenzi.
Mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akifanya ya kusimamia shamba la
mtu pamoja na kufanya kazi ya bodaboda anatuhumiwa kufanya mauaji hayo nyumbani
kwa wakwe zake baada ya kuona kuwa mkewe amegoma kwenda kwake kutokana na
ugomvi uliokuwepo baina yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu
mwenyekiti wa Kijiji cha Boko Mnemela Hassan Mohamed alisema kuwa tukio hilo
limetokea Julai 27 majira ya saa mbili asubuhi.
Mohamed alisema kuwa siku moja kabla ya tukio hilo Julai 26
mtuhumiwa huyo akiwa na amesindikizwa na mtu mmoja ambaye jina lake bado
halijapatikana walikuwa na kikao cha kusuluhishwa baada ya kuhitilafiana na kikoa hicho kilifanyika nyumbani kwa wazazi
wa marehemu.
“Kwa mujibu wa watu waliohudhuria kikao hicho walisema kuwa
kikao hicho kilifanyika kuanzia majira ya saa 2 usiku hadi saa 5 usiku ambapo
hata hivyo mwafaka haukuweza kufikiwa kwani marehemu alikataa kwenda kwa mume
wake,” alisema Mohamed.
Alisema kuwa siku iliyofuata watu waliokuwa wakihusika
kusuluhisha waliondoka na yeye pamoja na mtu aliyeambatana naye waliondoka
lakini ghafla alirudi akidai kuwa anafuata betri ya simu aliyoisahau nyumbani
kwao na marehemu.
“Alimkuta mkewe akipepeta mchele jikoni na kuanza
kumbembeleza lakini inaonekana aligoma kabisa kurudi kwa mumewe hali ambayo ili
mkasirisha mumewe na kuanza kumchoma kwa kutumia kisu huko jikoni kisha
wakatoana nje huku marehemu akipiga kelele,” alisema Mohamed.
“Mtuhumiwa alimchoma marehemu kwenye ziwa la upande wa kulia
na kwenye uti wa mgongo karibu na bega la upande wa kushoto na alimchoma kisu
mbele ya bibi yake mama yake wa kufikia na mdogo wake ambao walipiga kelele na
kushindwa kumsaidia ambapo mtuhumiwa huyo alikimbia maporini,” alisema Mohamed.
Mwenyekiti huyo alipoulizwa juu ya chanzo cha mauaji hayo
alisema kuwa kwa mujibu wa watu waliokuwa wakijua ugomvi wao walisema kuwa
mtuhumiwa alikerwa na tabia ya mkewe kurudishiwa zaidi chenchi anapokwenda
kwenye duka lililopo kijijini hapo.
“Marehemu alikuwa akimjulisha mumewe juu ya hali hiyo ambapo
inasemekana aligoma kurudi kutokana na kuambulia vipigo na kutishiwa kuuwawa na
mwanaume huyo na kupelekea kufanyika kikao cha usuluhishi na muuza duka kifanyike
ili kupata mwafaka lakini ikashindikana na kutokea mauaji hayo ya kusikitisha,”
alisema Mohamed.
Jitihada za kumpata kamanda wa Polisi mkoani Pwani Kamishna
Msaidizi Mwanadamizi wa Polisi Ulrch Matei hazikuweza kuzaa matunda ili aweze
kuzungumzia tukio hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment