Monday, July 28, 2014

AMWUA MKEWE KWA WIVU WA MAPENZI



KIJANA aliyetambuliwa kwa jina la Omary Molel mkazi wa Kijiji cha Mwanabwito kata ya Ruvu wilayani Kibaha mkoani Pwani anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (25) anatuhumiwa kumwua mchumba wake Sina Hamis (21) kwa kumchoma kisu kutokana na wivu wa mapenzi.

Mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akifanya kazi ya kusimamia shamba la mtu pamoja na kufanya kazi ya bodaboda anatuhumiwa kufanya mauaji hayo nyumbani kwa wakwe zake baada ya kuona kuwa mkewe amegoma kwenda kwake kutokana na ugomvi uliokuwepo baina yao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu mwenyekiti wa Kijiji cha Boko Mnemela Hassan Mohamed amesema kuwa tukio hilo limetokea Julai 27 majira ya saa mbili asubuhi.

Mohamed amesema kuwa siku moja kabla ya tukio hilo Julai 26 mtuhumiwa huyo akiwa na amesindikizwa na mtu mmoja ambaye jina lake bado halijapatikana walikuwa na kikao cha kusuluhishwa baada ya kuhitilafiana  na kikao hicho kilifanyika nyumbani kwa wazazi wa marehemu.

Amesema kuwa Kwa mujibu wa watu waliohudhuria kikao hicho wamesema kuwa kikao hicho kilifanyika kuanzia majira ya saa 2 usiku hadi saa 5 usiku ambapo hata hivyo mwafaka haukuweza kufikiwa kwani marehemu alikataa kwenda kwa mume wake.

Aidha amessema kuwa siku iliyofuata watu waliokuwa wakihusika kusuluhisha waliondoka na yeye pamoja na mtu aliyeambatana naye waliondoka lakini ghafla alirudi akidai kuwa anafuata betri ya simu aliyoisahau nyumbani kwao na marehemu.

Alimkuta mkewe akipepeta mchele jikoni na kuanza kumbembeleza lakini inaonekana aligoma kabisa kurudi kwa mumewe hali ambayo ili mkasirisha mumewe na kuanza kumchoma kwa kutumia kisu huko jikoni kisha wakatoana nje huku marehemu akipiga kelele.

Ameongeza kuwa Mtuhumiwa alimchoma marehemu kwenye ziwa la upande wa kulia na kwenye uti wa mgongo karibu na bega la upande wa kushoto na alimchoma kisu mbele ya bibi yake mama yake wa kufikia na mdogo wake ambao walipiga kelele na kushindwa kumsaidia ambapo mtuhumiwa huyo alikimbia maporini.

Mwenyekiti huyo alipoulizwa juu ya chanzo cha mauaji hayo amesema kuwa kwa mujibu wa watu waliokuwa wakijua ugomvi wao walisema kuwa mtuhumiwa alikerwa na tabia ya mkewe kurudishiwa zaidi chenchi anapokwenda kwenye duka lililopo kijijini hapo.

Ameongeza kuwa Marehemu alikuwa akimjulisha mumewe juu ya hali hiyo ambapo inasemekana aligoma kurudi kutokana na kuambulia vipigo na kutishiwa kuuwawa na mwanaume huyo na kupelekea kufanyika kikao cha usuluhishi na muuza duka kifanyika ili kupata mwafaka lakini ikashindikana na kutokea mauaji hayo ya kusikitisha.

Kwa upande wa kamanda wa Polisi mkoani Pwani Kamishna Msaidizi Mwanadamizi wa Polisi (SACP) Ulrich Matei amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa huyo anatafutwa ambapo jitihada hizo bado hazijazaa matunda.

 

  

No comments:

Post a Comment