Na John Gagarini, Kibaha
HATIMAYE ule mgomo wa wachinjaji ngombe
na wamiliki wa mabucha wilayani Kibaha mkoani Pwani umekwisha baada ya pande
mbili zilizokuwa zikitofautia Halmashauri ya Mji wa Kibaha na wamiliki wa
mabucha hayo chini ya mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba kukaa meza moja
na kumaliza mgomo huo uliodumu kwa muda wa siku mbili kuanzia Julai 18 hadi 19.
Mgomo huo ambao uliendeshwa na wamiliki
hao wa mabucha ambao ndiyo wachinjaji wa ng’ombe kupitia Umoja wa
wafanyabiashara wa nyama na mazao yake wilayani Kibaha (UWABINK)
walifanya mgomo wa kuuza nyama kwa mji wa Kibaha na vitongoji vyake kwa madai
kuwa machinjio mpya ya Mtakuja waliohamishiwa haina huduma muhimu ikiwemo maji
huku wakitaka kutumia ile ya zamani ya Maili Moja.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi
jana mjini Kibaha kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya Kibaha Kihemba alisema
kuwa kulitokea tofauti baina ya pande hizo mbili hali iliyosababisha mgomo huo
ambao uliathiri walaji wa nyama wa mji huo na maeneo ya wilaya ya Kinondoni
Jijini Dar es Salaam.
Kihemba alisema kuwa suala la maji
pande hizo zimekubaliana Halmashauri watanunua maji kwa kipindi cha wiki moja
na UWABINK nao watanunua wiki moja hivyo watapeana zamu ya kununua maji hadi
suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi ambapo halmashauri imetenga kiasi cha
shilingi milioni 19 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu cha maji Septemba mwaka
huu.
“Muafaka ni kwamba waendelee kuchinja
kwenye machinjio ya zamani kwa muda wa siku tatu kuanzia Julai 20 hadi Julai 22
kisha wahamie kule, kwani kwa kipindi hicho taayari marekebisho yatakuwa
yamefanywa na maji watashirikiana kununua,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa baada ya siku tatu
watatakiwa hamie huko machinjio mpya na ile ya zamani itabomolewa ili kupisha
shughuli nyingine kwenye eneo hilo hivyo anaamini muafaka huo utaondoa msuguano
uliojitokeza.
“Kuhusu zizi walikuwa hawajajenga hivyo
wajenge zizi hilo katika kipindi hicho walichokubaliana ambapo waliingia
mkataba wa uendeshaji ambapo wao wanachinja halmashauri wao ni wa miliki wa miuondombinu
na wao hulipa ushuru kwa kila mwezi ni zaidi ya shilingi milioni moja,” alisema
Kihemba.
Kwa upande wake msemaji wa umoja huo
Athumani Mkanga alisema waliamua kufanya mgomo huo kupinga kuhamishiwa
kwenye machinji hayo ya Mtakuja kutoka yale ya Maili Moja kwani yalikuwa
hayajakamilika na hayakuwa na huduma muhimu ikiwemo maji na umeme ambapo ule wa
jua hautakidhi mahitaji yao.
Mkanga alisema kuwa walikaa meza moja
na halmashauri chini ya mkuu wa wilaya ambaye alikuwa mwenyekiti na kukubaliana
kuwa watashirikiana katika masuala mbalimbali kwenye machinjio hayo mapya.
“Tumekubaliana baadhi ya mambo ikiwemo
sula la maji ambapo tutayanunua kwa zamu wakati wao wanaendelea na utaratibu wa
kuchimba kisima kirefu ili kukabiliana na tatizo la maji na masuala mengine,”
alisema Mkanga.
Alibainisha kuwa wamekubaliana na
marekebisho hayo lakini wanachokitaka ni kuboreshwa kwa huduma ili waweze
kufanya shughuli zao bila ya kikwazo chochote lengo likiwa ni kutoa huduma bora
kwa walaji.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment