Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa ucheleweshaji wa ubadilishaji wa sheria
kandamizi kwa wanawake na watoto hapa nchini kumechangia kiasi kikubwa
kuendelea vitendo vya unyanyasaji wa makundi hayo ndani ya jamii.
Sheria hizo ambazo zilitungwa miaka ya nyuma zinaonekana
kuyakandamiza makundi hayo ambayo yanaonekana ni manyonge ndani ya jamii kwani
watu wameendeleza kuyakandamiza hasa katika mgawanyo wa mali.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na Jane Mgaigita mwezeshaji
wa mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na kituo cha msaada wa Kisheria kwa
wanawake (WLAC) kwa wadau wa kituo hicho wakiwemo maakimu, watendaji wa mitaa
na kata pamoja na polisi, wilaya ya Kibaha mkoani Pwani juu ya haki za wanawake.
Magigita alisema kuwa baadhi ya sheria ni kandamizi ambazo
inapaswa zibadilishwe ili makundi hayo yaweze kupata haki zao hasa pale
inapofikia wakati wa mgawanyo wa mali.
“Wanawake wengi na watoto wamekuwa wakikandamizwa na sheria
hizo zikiwemo zile za ndoa na masula ya mirathi ambazo bado zinatumiwa na Mahakama
zikiwemo zile za mwanzo hivyo ni vema zikarekebishwa ili kuondoa unyanyasaji
ndani ya jamii,” alisema Magigita.
Alisema kuwa wao kama wanaharakati wamekuwa wakipeleka
mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hizo kandamizi ili zibadilishwe lakini
zimekuwa hazifanyiwe marekebisho na kuwafanya wanajamii hao kuzidi kukandamizwa
kutokana na hali hiyo.
“Baadhi ya sheria za masuala mengine zimekuwa zikirekebishwa
harakaharaka lakini hizi za wanawake
hazipewi nafasi kabisa na kufumbiwa macho hivyo kuendeleza unyanyasaji, ”
alisema Magigita.
Kwa upande wake hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa wa Pwani Salome
Mshasha alisema kuwa mbali ya changamoto hiyo ya sheria pia baadhi ya wanawake
wamekuwa wakikata tamaa na kuacha kutoa taarifa juu ya haki zao.
“Baadhi ya wanawake wamekuwa wakijirudisha nyuma kwenye suala
la kudai haki zao jambo ambalo linawafanya wasipate haki na kuwaacha wanaume
wakijinufaisha,” alisema Mshasha.
Naye mwenyekiti wa baraza la Ardhi la wilaya ya Kibaha Maketa
Bigambo alisema kuwa wao kama wadau wa utoaji haki watahakikisha kila kundi
linapata haki yake ili kuondoa malalamiko hayo.
Bigambo alisema jambo ambalo linatakiwa ni pamoja na wanake
kutokata tamaa kufuatilia haki zao kwenye vyombo vinavyohusika ili kukabiliana
na ukandamizaji unaofanywa na baadhi ya wanafamilia.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment