Friday, July 18, 2014

RIDHIWANI ATOA MSAADA POLISI



Na John Gagarini, Chalinze

KATIKA kuhakikisha Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa teknolojia ya kisasa Mbunge wa jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani  Ridhiwani Kikwete ametoa msaada wa kompyuta na mashine za kutolea kopi zenye thamani ya shilingi milioni 11 kwa kanda maalumu ya kipolisi ya Wilaya ya Chalinze.

Msaada huo wa kompyuta, na mashine ya kutolea kopi utasaidia kuhifadhi nyaraka za kipolisi na pia kuachana na usumbufu wa kutumia steshenari zilizopo nje ya ofisi yao.

Akikabidhi msaada huo wa kompyuta pamoja na fedha taslimu kwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Pwani Ulrich Matei, Ridhiwani alisema lengo ni uboreshaji wa vituo vya polisi katika jimbo hilo.

“Kwa kuwa kituo hichi cha polisi Chalinze kimepandishwa hadhi na kuwa cha wilaya bado kinakabiliwa na changamoto ya uwepo wa ofisi ndogo ambayo haikidhi mahitaji na kusababisha kutumia kontena kufanyia kazi nyingine za kiofisi nimetoa kwa ajili ya siri za kiofisi badala ya kufanyia kazi nje ya kituo,” alisema Ridhiwani.

Ridhiwani alisema kuwa siri nyingi za ofisi zilikuwa zikivuja kutokana na kazi kufanyiwa nje ya ofisi jambo ambalo lilikuwa likisababisha uvujaji wa taarifa hivyo kushindwa kufanikiwa kudhibiti uhalifu kikamilifu.

Kwa upande wake  Kamanda Matei  alimshukuru mbunge huyo na kusema kuwa kituo cha Chalinze ambacho kimepandishwa hadhi na kuwa cha kiwilaya kwasasa ni kipya na
hivyo kinahitaji maboresho mengi ambapo aliahidi kudumisha ushirikiano ili kusaidiana katika kutatua changamoto nyingine za vituo hivyo.

Naye Diwani wa kata ya Bwilingu Nasa Karama alimueleza mbunge huyo kuwa  tangu kituo hicho kipandishwe hadhi na kuwa cha wilaya, shughuli nyingi zimeongezeka na hivyo kuwa na kazi kubw aya kuzuia uhalifu

“Tunashukuru kwa msaada huu pia tunaomba msaada wa kujengewa nyumba kwa ajili askari kwani wengi wa kituo hicho hawana nyumba za kuishi na hivyo kulazimika kupanga uraiani na kusababisha utendaji kazi kupungua.

Misaada iliyokabidhiwa kwa jeshi hilo ni pamoja na shilingi Milioni
tatu kwa ajili ya kituo cha polisi Mbwewe, mifuko ya saruji 20 na
shilingi 350,000 kwa ajili ya kuharakisha ujenzi wa kituo cha polisi
Kiwangwa pamoja na kompyuta na mashine ya kutolea kopi kwa ajili ya
kituo cha Chalinze.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment