Sunday, July 27, 2014

MAGUFULI ATOA UFAFANUZI WA FIDIA BARABARA NDUNDU SOMANGA



Na John Gagarini, Rufiji
Serikali kupitia wizara ya Ujenzi imetoa ufafanuzi juu ya suala la fidia kwa wakazi wanaopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya Ndundu-Somanga iliyopo kati ya Mikoa ya Pwani na Lindi.
Waziri wa ujenzi Pombe Magufuli akizungumzia suala hilo kwa wananchi wakati akikagua barabara hiyo huku akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali,wakala wa Tanroads katika Mikoa ya Lindi na Pwani alisema wale waliojenga nyumba zao ndani ya mita 22.5 hawatolipwa fidia kutokana na kuvunja sheria.
Alieleza kuwa mbali ya kutolipwa fidia pia watu hao watatakiwa kulipia gharama za mafuta ya greda ambalo litafanya kazi ya ubomoaji.
Magufuli Alielezea wale walio nje ya mita 22.5 na ambao makazi yao yamejengwa nyuma ya mwaka 2007 ambapo watawekewa alama ya X kwa rangi ya kijani ikiashiria hao ndio watalipwa fidia .
Aidha Waziri huyo wa Ujenzi alikemea tabia ya kuiba mafuta inayofanywa na baadhi ya watumishi wa mkandarasi huyo sanjali na baadhi ya wananchi kwani kwa kufanya hivyo ni kukwamisha kasi ya ujenzi wa barabara hiyo.
Alitoa rai hiyo baada ya kufikishiwa malalamiko hayo na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Manzese kilicho mpakani mwa mikoa ya Lindi na Pwani kuwa kuna tabia ya kuibiwa mafuta jambo ambalo linasababisha ujenzi kusuasua.
Magufuli pia alimtaka mkandarasi wa barabara hiyo M.A Kharafi $ Sons Ltd kuwalipa fedha nzuri wafanyakazi wake  ili waweze kuondokana na tamaa za kuiba mafuta na vifaa vingine.
Mwishoni mwa wiki Magufuli alitoa siku 60 kwa Mkandarasi wa barabara ya Ndundu-Somanga iliyopo kati ya Mikoa ya lindi na Pwani M.A Kharafi $Sons Ltd kuhakikisha anamaliza ujenzi wa barabara hiyo .
Agizo hilo ni kuanzia sasa hadi mwezi wa 9 mwaka huu awe ameshamaliza kazi hiyo na kama akizembea serikali itamchukulia hatua zaidi kwani imeshamlipa kwa awamu nyingine Bil 8.91 hivyo hakuna kisingizio kingine.

Waziri Magufuli alisema mkandarasi huyo amekiuka mkataba hivyo serikali imechoshwa na usumbufu na visingizio vyake  .
Alisema Mkataba wake ulikuwa ukionyesha kuanza ujenzi mwaka 2009 na kukamilika 2011 kwa kujenga km 56.318 kwa kiwango cha lami lakini hadi sasa km 10 bado hajazikamilika.
Sambamba na agizo hilo aliwaagiza mameneja wa wakala wa barabara Tanroads ,Mikoa ya Lindi na Pwani kumbana Mkandarasi huyo ili kuhakikisha hazembei kumaliza kazi hiyo kwa muda aliopewa.
Aidha alisema tayari kwasasa wizara imechukua hatua ya kumfukuza kazi Mhandisi Msimamizi ushauri wa awali wa ujezi wa barabara hiyo Engineering System Group –KSCC toka juni 8 mwaka huu .
Ambapo kwasasa barabara hiyo itasimamiwa na Wakala wa barabara –Tanroads-yenyewe kupitia kitengo cha usimamizi wa kazi ndani ya wakala huo kwa mujibu wa sheria namba 16 ya mwaka 1997.

"Wasimamiazi hao wamsimamie mkandarasi hadi atoke makamasi ,na ni lazima kuanzia sasa afanye kazi usiku na mchana,jumatatu hadi jumapili ili amalize ujenzi kwa muda wa miezi hii miwili pekee”alisema Magufuli.

Alieleza kuwa ifikie hatua ya kusema basi kulea wakandarasi wasumbufu ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo vumbi na kukwama kwa magari kutokana na uzembe wa mkandarasi husika.

Nae Mtendaji Mkuu wa wakala wa barabara Tanroads nchini ,Mhandisi Patrick Mfugale alieleza mbali ya changamoto hiyo pia mkandarasi huyo alishindwa kuendesha mradi kwa fedha zake mwenyewe hadi serikali ilipomwezesha.
Sababu nyingine ni kucheleweshwa kwa fedha kutoka kwa wachangiaji wa fedha wengine katika mradi huo ikiwemo OPEC na Quwait fund .
Barabara ya Ndundu-Somanga  ina urefu wa km 56.318 ,zilizokamilika ni km 42 huku km 10 zikiwa bado hazijakamilika,na hadi kukamilika kwa ujenzi itagharimu kiasi cha sh. Bil 58.813 ambapo hadi sasa umegharimu sh.Bil 49.
Katika gharama hizo serikali itachangia asilimia 55,OPEC 14 na Quwait Fund asilimia 31.

Mwisho

No comments:

Post a Comment