Wednesday, November 22, 2017

PWANI WATAKA WATAALAMU WA UWEKEZAJI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Zuberi Samataba ambaye aliongoza ujumbe wa viongozi na wataalamu waliotembelea nchi ya China akiongea

Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani Zuberi Samataba akielezea jambo kulia ni mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo  


 Baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa wa Pwani kuanzia kushoto Gulmahusein Kifu wilaya ya Kibiti anayefuata Happyness Seneda wilaya ya Kisarawe, Juma Njwayo wilaya ya Rufiji  na Majid Mwanga wilaya ya Bagamoyo

 Baadhi ya washiriki wakijadili baada ya kupokea taarifa ya baadhi ya viongozi na wataalamu waliotembelea nchi ya China 

Na John Gagarini, Kibaha

WATAKA kuwekwa wataalamu wa uwekezaji kwenye kila Halmashauri mkoani humo ili kuwawekea mazingira mazuri ya mawasiliano na wawekezaji.

Ushauri huo ulitolewa mjini Kibaha na baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa huo wakati wa kupokea taarifa toka kwa timu ya wataalamu na viongozi wa mkoa na Halmasahuri ya wilaya ya Kibaha waliokwenda nchini China.

Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga alisema kuwa wataalamu hao wakiajiriwa itasaidia kurahisisha wawekezaji kuwa na mtu maalumu ambaye atakuwa anawajibika kwa wawekezaji wanaokuja mkoani humo.

“Kukiwa na dawati maalumu kwa ajili ya wawekezaji itasaidia kupunguza usumbufu wa mwekezaji kuzungushwa wakati wa kupata vibali mbalimbali vya uwekezaji,” alisema Sanga.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kisarawe Happynes Seneda alisema kuwa mtaalamu huyo atakuwa akiwajibika na suala la wawekezaji kwani kwa sasa nchi imehamasisha ujengwaji wa viwanda hivyo kutakuwa na wageni wengi toka nje ya nchi kwa ajili ya uwekezaji.

Seneda alisema kuwa mtaalamu atajua masuala mbalimbali yanayohusiana na uwekezaji kuanzia masuala ya ardhi, upatikanaji wa vibali mbalimbali na kuwa na mawasiliano na sekta wezeshi kwa ajili ya kutatua changamoto kwa wawekezaji.      

Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa madawati ya wataalamu wa uwekezaji kwenye Halmashauri pia sekta wezeshi zinapaswa kuwa na wtu watakaokuwa wanahusika na wawekezaji.

Ndikilo alisema kuwa sekta wezeshi kama vile TANESCO, CHALIWASA, DAWASCO, TARURA, TRA, Polisi na Uhamiaji lazima inakuwa na watu wanaofanya kazi ya kushughulikia wageni.

“Tukiwa na wataalamu wa kudili na wageni itakuwa rahisi kutoa huduma kwa haraka na kwa wakati pia itasaidia kuondoa urasimu wakati wa kuwahudumia wawekezaji ili waweze kutekeleza majukumu yao,” alisema Ndikilo.


Mwisho.

Thursday, November 16, 2017

WENGI WAMWAGA ALBERT NGWADA




Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani Anastazia Amas akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Albert Ngwada kwenye ofisi za CCM Kibaha Mjini.

 Baadhi ya waombolezaji wakiaga mwili wa Ngwada



 Baadhi ya waombolezaji wakiangua vilo baada ya kuuaga mwili wa Ngwada

Vijana wa CCM wakiwa wamebeba jeneza lililokuwa na mwili wa Ngwada 


 Mama wa Marehemu katikati akiwa anabembelezwa wakati wa kuaga mwili wa mwanae kwenda mkoani Iringa kwa ajaili ya mazishi.
 Katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu akitoa taarifa fupi ya marehemu wakati wa kuaga kwenye ofisi za CCM Kibaha Mjini 
Na John Gagarini, Kibaha

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani Anastazia Amas juzi aliwaongoza wanachama na wananchi wa wilaya ya Kibaha kuaga mwili wa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoa wa Pwani kuwakilisha Kata ya Pangani Albert Ngwada kwa ajili ya mazishi mkoani Iringa ambaye alifariki dunia Novemba 13 mwaka huu.

Akiongea wakati wa kuaga mwili wa marehemu Ngwada kwenye ofisi za CCM Kibaha Mjini Amas alisema kuwa chama kimepata pigo kutokana na kifo hicho cha mjumbe wa CCM.

Amas alisema kuwa ili kumkumbuka marehemu wanachama wanapaswa kufanya kazi za chama kwa uaminifu na uadilifu ili kuleta maendeleo ndani ya chama na kwa wananchi wa Kibaha kama alivyokuwa Ngwada.

“Natoa pole kwa ndugu na wote walioguswa na msiba huu ambao umewagusa watu wengi na ndiyo maana watu wamejaa hii yote inaonyesha jinsi gani mlivyokuwa mnamkubali kutokana na utendaji wake kikubwa ni kuenzi utendaji wake,” alisema Amas.  

Awali akitoa maelezo mafupi juu ya marehemu katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa kutokana na utendaji wake kazi mzuri marehemu alipandishwa cheo kutoka Katibu msadizi wa kata ya Pangani na kuwa kaimu katibu msaidizi wa CCM Kibaha Mjini mwaka 2015

Mdimu alisema kuwa marehemu alitumikia nafasi hiyo kama msiadizi wake hadi mwaka 2017 baada ya kuletwa katibu msaidizi toka Magu ambapo Aprili alichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa toka kata ya Pangani nafasi aliyokuwa nayo hadi anafariki dunia.

Awali marehemu alianza kukitumikia chama mwaka 2007 hadi mwaka 2012 alipochaguliwa kuwa katibu kata Pangani hadi 2017 Juni 2015 alipanda daraja na kuwa Kaimu katibu Msaidizi hadi Aprili 2017.

Alisema kuwa mwaka huu mwezi Mei alichaguliwa kuwa Mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa kupitia kata ya Pangani  na tarehe 4 Oktoba alipata ajali ya Pikipiki huko eneo la Kidimu majira ya saa 1:30 usiku na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani ya Tumbi na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Aidha marehemu alifariki dunia wakati akiendelea na kliniki baada ya kutolewa Hospitali na alitarajiwa kuzikwa jana kwao mkoani Iringa na alizaliwa mwaka 1982.

Mwisho.
















UINGIZAJI MIFUGO TOKA NJE YA NCHI SERIKALI YASHAURIWA






Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI imetakiwa iendee kudhibiti uingizaji mifugo kutoka nje ya nchi ili kuepuka magonjwa ambayo yakiingia yataathiri soko la nje ambalo linapato kubwa.

Hayo yalisemwa wilayani Kibaha na Mwenyekiti wa Chama Cha Waganga Wasaidizi wa Mifugo Tanzania (TAVEPA) Salim Mselem wakati wa mkutano wa kamati kuu ya chama hicho na kusema kuwa lazima kuwe na udhibiti wa magonjwa.

Mselem alisema kuwa suala la udhibiti wa magonjwa ni mgumu sana lakini serikali kwa kushirirkrana na wataalamu wake wanapaswa kudhibiti uingizwaji wa mifugo hapa nchini.

“Hivi karibuni serikali ilivichoma moto vifaranga ambavyo viliingizwa kwenye mpaka wa Namanga ambapo wahusika hawakufuata taratibu za uingizaji mifugo na hizo ndiyo sheria hata kwenye mataifa mengine,” alisema Mselem.

Alisema kuwa ili kudhibiti magonjwa lazima mifugo inayoingia nchini lazima ikaguliwe ili kuangalia kama imepata chanjo na kama haijapata chanjo lazima uharibiwe.

“Magonjwa mengine ni ya hatari sana licha ya kuathiri soko la nje ambapo endapo itabainika mifugo yetu ina maganjwa haitaruhusiwa kwenye nchi za nje hata kwa afya za walaji pia ni hatari sana na hatutakubali nchi yetu kuwa sehemu ya kuuzwa vitu vibaya,” alisema Mselem.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa TAVEPA Ephrahim Masawe alisema kuwa kitengo cha ukaguzi wa uingizwaji mifugo kinapaswa kuwa makini ili kuepuka uingizwaji wa mifugo ambayo haijachanjwa.



Masawe alisema kuwa mifugo inayo ingizwa bila ya kuchanjwa ina hatari ya kuingiza magonjwa ambayo ni ya hatari kwa mifugo pamoja na afya za walaji.

Mwisho.




Friday, October 27, 2017

MIILI MIWILI YA WATU WALIOSOMBWA NA MAJI YAPATIKANA


Na John Gagarini, Kibaha

WATU wawili wamefariki dunia kufutaia mvua iliyonyesha juzi mkoani Pwani ambapo miili yao imeweza kugundulika baada ya maji kupungua kwenye mto Mpiji unaotenganisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Akithibitisha kuokotwa kwa miili hiyo kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Blasius Chatanda alisema kuwa miili hiyo ilikutwa kando kando ya mto huo ambao ulikuwa umejaa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali ya nchi.

Chatanda alisema kuwa miili hiyo ilokotwa maeneo tofauti ambapo mwili wa kwanza ulipatikana majira ya saa 2:30 eneo la Muheza kata ya Pangani alitambuliwa kwa jina la Simon Ramadhan mwenye umri kati ya miaka (25) na (30) uliokotwa eneo la mto Mpiji na marehemu alikufa alipokuwa akijaribu kuvuka.

“Mwili wa pili wa Issa Ally (28) ambaye ni mgambo uliokotwa eneo la Kiluvya na inadaiwa kuwa marehemu alisombwa na maji alipokuwa akijaribu kumwokoa mtoto aliyetaka kusombwa na maji na kukutwa kilometa nne toka sehemu aliyozama,” alisema Chatanda.

Alisema kuwa miili yote ya marehemu imehifadhiwa kwenye hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa ajili ya kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.

“Nawaomba wananchi kuwa makini wakati wa kuvuka kwenye mito kuwa na subira ili maji yapungue waweze kuvuka na kuendelea na safari zao kwani wasidaharu maji kama ni madogo ambapo yanaweza kuwaletea madhara,” alisema Chatanda.

Mwisho.   
  


SABA WASOMBWA NA MAJI WANUSURIKA


Daraja linalounganisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam likiwa limejaa maji

 Baadhi ya wananchi wakifuatilia zoezi la uokoaji watu waliosombwa na maji ambao walipanda kwenye miti

 Moja ya kijana aliyenusurika Silas Moshi baada ya kusombwa na maji mara baada ya kuokolowa

 Dada ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja baada ya kuokolewa akiwa amepoteza fahamu akipakiwa kwenye gari la polisi kwa ajili ya huduma ya kwanza.



 Kijana Mohamed Kitindi aliyenusurika baada ya kusombwa na maji 

 Furaha Mwaipopo moja ya watu walionusurika baada ya kusombwa na maji na kupanda kwenye mti


 Moja ya watu walionusurika akihojiwa na polisi baada ya kunusurika 

 Kened Meshaki ambaye alishika nguzo ya bango huku mwili wake ukiwa ndani ya maji kwa zaidi ya masaa matatu akiwa ameshikwa mkono na polisi kwa ajili ya kwenda kupatiwa huduma ya kwanza


Na John Gagarini,Kibaha

WATU saba wamenusurika kifo baada ya kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka huku wakiwa wameshikana mikono ambapo walijinusuru kwa kupanda kwenye miti kabla ya kuokolewa na kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani.

Aidha kati ya watu hao mmoja alikuwa akininginia kwa kujishika kwenye bomba la bango la matangazo huku mwili wake ukiwa ndani ya maji kwa masaa zaidi ya huku akiwa anaomba msaada wa kuokolewa bila mafanikio.

Watu walionusurika ni pamoja na Kened Meshaki, Mohamed Kitindi, Silas Moshi Henry Francis na mwanamke mmoj ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja ambao wote walikimbizwa hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Pwani.

Tukio hilo lilitokea jana eneo la Maili Moja wilayani Kibaha kwenye daraja linalotenganisha kati ya mkoa wa Dar es Salaam na mkoa wa Pwani na kusababisha daraja kujaa maji na kusababisha magari na watu kushindwa kuvuka upande wa pili.

Daraja hilo ambalo linapita kwenye mto Mpiji lilikuwa halipitiki na kusababisha watu na abiria kushindwa kuvuka upande wa pili kutoka Maili Moja wilayani Kibaha na upande mwingine Kiluvya wilaya ya Ubungo.

Kutokana na daraja hilo kushindwa kupitika abiria wa mabasi wameshindwa kuendelea na safari zao za kwenda mikoani na maeneo mengine yanayopita kwenye barabara ya Morogoro.

Akizungumza na gazeti hili kwenye eneo la tukio hilo ofisa habari na uhusiano wa Jeshi la uokoaji Harison Mkonyi alisema kuwa zoezi la ukoaji limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani wameweza kuwaokoa watu hao wakiwa salama.

Mkonyi alisema kuwa wamefanikiwa kuwaokoa watu hao kwa kushirikiana na wadau wengine ambao walijitosa kwenye maji hayo ambayo yalikuwa mengi na kulifunika kabisa daraja hilo na kusababisha kushindwa kupitika.

“Tunawashukuru wadau mbalimbali vikiwemo vikosi vya majeshi ya Polisi, Magereza, JWTZ na wananchi ambao walionyesha ushirikiano wa hali ya juu kuwanusuru watu hao akiwemo mwanamke mmoja,” alisema Mkonyi.

Mwisho.

Thursday, October 19, 2017

MBUNGE KIBAHA MJINI AKABIDHI VYEREHANI KWA WATU WENYE ULEMAVU


Na John Gagarini, Kibaha

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha mkoani Pwani Silvestry Koka ametoa vyerehani vinnne kwa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) wilaya ya Kibaha kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.

Akikabidhi vyerehani hivyo kwa uongozi wa shirikisho hilo Katibbu wa Mbunge huyo Method Mselewa alisema kuwa mbunge huyo katoa vyerehani hivyo kufuatia ombi lao.

Mselewa alisema kuwa watu wenye ulemavu nao wanapaswa kusaidiwa kama wanavyosaidiwa watu wa makundi mengine yanavyosaidiwa ili kujiendeleza kiuchumi.

“Kuwa na ulemavu siyo mwisho wa maisha kwani nguvu mnazo na mnauwezo kama watu wasiokuwa na ulemavu na tutaendelea kuwasaidia ili nanyi mjikwamue kwa kujiongezea kipato chenu na cha familia zenu,” alisema Mselewa.

Alisema kuwa kutokana na kuungana kwao kutasaidia kuwafikia kwa urahisi kuliko kila mtu angekuwa anaomba peke yake ingekuwa ngumu lakini kwa kuwa pamoja imekuwa rahisi.

“Hizi mashine mnapaswa kuzitunza kwani mbali ya kuwapatia ujuzi kia zitawapatia kipato ambacho kitaweza kuwafanya muwe na mapato kuliko kuomba jambo ambalo halifurahishi,” alisema Mselewa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa SHIVYAWATA Ally Mlanga alisema kuwa wanshukuru msaada huo kwani kwao huo ni kama mtaji ambao watahakikisha wnaauendeleza.

Mlanga alisema kuwa wao hawataki fedha ila wanachotaka ni kupewa vitu ambavyo vitawasaidia kuliko fedha ambazo zinaweza kupotea kwa urahisi.

Naye ofisa Maendeleo wa Kata ya Kibaha Regina Lazaro alisema kuwa kupatiwa vyerehani hivyo vitawasaidia kujiongezea kipato kwani moja ya shughuli zake ni kuhamasisha ujasiriamali.

Lazaro alisema kuwa wamekuwa wakishirikiana na shirikisho hilo ikiwa ni njia mojawapo ya kuwasaidia kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na serikali au wadau toka sekta binafsi.


Mwisho.

WAWILI WASHIKILIWA NA POLISI KWA KUKUTWA NA MAGUNIA SABA YA BHANGI



Na John Gagarini, Kibaha


WATU wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Pwani kwa tuhuma za kukutwa na magunia saba ya dawa za kulevya aina ya bhangi yenye uzito wa kilogramu 7,500.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Jonathan Shana alisema kuwa watuhumiwa hao waligundulika baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali.

Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea huko Kwa Mathias wilaya ya Kibaha baada ya askari waliokuwa doria kupata taarifa juu ya ajali ya gari.

“Watuhumiwa hao walikuwa kwenye gari namba T847DHT aina ya IST ambalo lilipata ajali kwenye eneo hilo na baada ya kufika walianza kuwaokoa na ndipo walipokuta na gunia saba za bhangi hiyo ikiwa kwenye hilo gari ikiwa imehifadhiwa kwenye magunia ya salfeti,” alisema Shana.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kundaeli Mbowe (24) ambaye ni dereva wa gari hilo na mkazi wa Kiwalani Jijini Dar es Salaam na Ally Mtena (28) mfanyabiashara na makazi wa Gongolamboto.

Aidha alisema kuwa watuhumiwa hao wanashikiliwa ili kuweza kuchukuliwa hatua za kisheria na kujua bhangi hiyo waliitowa wapi na walikuwa wakiipeleka wapi.


Mwisho.