Friday, October 27, 2017

MIILI MIWILI YA WATU WALIOSOMBWA NA MAJI YAPATIKANA


Na John Gagarini, Kibaha

WATU wawili wamefariki dunia kufutaia mvua iliyonyesha juzi mkoani Pwani ambapo miili yao imeweza kugundulika baada ya maji kupungua kwenye mto Mpiji unaotenganisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Akithibitisha kuokotwa kwa miili hiyo kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Blasius Chatanda alisema kuwa miili hiyo ilikutwa kando kando ya mto huo ambao ulikuwa umejaa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali ya nchi.

Chatanda alisema kuwa miili hiyo ilokotwa maeneo tofauti ambapo mwili wa kwanza ulipatikana majira ya saa 2:30 eneo la Muheza kata ya Pangani alitambuliwa kwa jina la Simon Ramadhan mwenye umri kati ya miaka (25) na (30) uliokotwa eneo la mto Mpiji na marehemu alikufa alipokuwa akijaribu kuvuka.

“Mwili wa pili wa Issa Ally (28) ambaye ni mgambo uliokotwa eneo la Kiluvya na inadaiwa kuwa marehemu alisombwa na maji alipokuwa akijaribu kumwokoa mtoto aliyetaka kusombwa na maji na kukutwa kilometa nne toka sehemu aliyozama,” alisema Chatanda.

Alisema kuwa miili yote ya marehemu imehifadhiwa kwenye hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa ajili ya kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.

“Nawaomba wananchi kuwa makini wakati wa kuvuka kwenye mito kuwa na subira ili maji yapungue waweze kuvuka na kuendelea na safari zao kwani wasidaharu maji kama ni madogo ambapo yanaweza kuwaletea madhara,” alisema Chatanda.

Mwisho.   
  


No comments:

Post a Comment