Sunday, October 8, 2017

WAANDISHI WA HABARI NCHINI WAASWA










Na John Gagarini, Kibaha

WAANDISHI wa Habari mkoani Pwani na hapa nchini wametakiwa kutotumia vibaya kalamu zao ili kulinda amani ya nchi kwani maneno yao endapo yatatumika vibaya ni hatari zaidi ya bunduki.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa wilaya ya Kibaha Asumter Mshama wakati akifungua kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani mafunzo juu ya Haki za Binaadamu Utawala Bora na Amani nchini kwa Viongozi na watumishi wa serikali za mitaa mkoa wa Pwani yaliyoandaliwa na Alpha And Omega Reconciliation And Peace Building (AREPEB).

Mshama alisema kuwa waandishi wana nafasi kubwa ya kudumisha amani iliyopo kwa kutumia vyema kalamu zao katika kuleta mshikamano na kuepusha utengano.

“Nyie ndiyo mnanafasi kubwa ya kuifanya nchi iendelee kuwa na amani au mnaweza kuifanya nchi ikaingia kwenye machafuko hivyo mnatakiwa kutumia vizuri kalamu zenu kwa kutotumia vibaya kalamu zenu,” alisema Mshama.

Alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia viongozi hao kuwahamasisha wananchi kulinda amani ya nchi na kutokubali kuingia kwenye migogoro ambayo itasababisha amani kuvunjika.

“Tanzania bado tuna amani kubwa na ya kutosha hatuna sababu ya kuleta vurugu kwani nchi inatawaliwa kwa utawala wa sheria lakini kuna baadhi ya watu wanataka kutuingiza kwenye matatizo,” alisema Mshama.

Naye mkurugenzi wa  (AREPEB) Francis Luziga alisema kuwa lengo lao kubwa ni kujenga amani hapa nchini kwa kubadilishana uzoefu na viongozi na watendaji wa serikali za mitaa na wasimamizi wa watekelezaji wa sheria katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora.

Luziga alisema kuwa pia mafunzo hayo yameambatana na uzinduzi wa mfumo wa kieletroniki wa kupokea maoni na malalamiko dhidi ya masuala mazima ya haki za binadamu.


Mwisho. 

No comments:

Post a Comment