Monday, October 9, 2017

ATAKA WATHAMINI RAIS KUREJESHA RASILIMALI ZA NCHI




Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha Asumter Mshama amesema anasikitishwa na watu wanaomsema vibaya Rais Dk John Magufuli kwa kutothamini kile anachokifanya katika kurejesha rasilimali za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha alisema kuwa kazi inayofanywa na Rais inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania yoyote anayeitakia mema nchi yake.
Mshama alisema kuwa kutokana na jitihada anazozifanya wananchi wanapaswa kumuunga mkono kwa kubainisha wale ambao hawana uzalendo na nchi yao.
“Rais kasikia kero nyingi na sasa ameanza kutekeleza kwa vitendo mfano masuala ya usafiri, upatikanaji wa dawa, suala la madini, reli na masuala ya viwanda iweje watu waanze kumsemea vibaya na kumwita majina yasiyofaa jambo hili halikubaliki,” alisema Mashama.
Alisema kuwa kuna njia nzuri za kumfikishia ujumbe hata kama unaona anakosea lakini siyo kumwambia maneno mabaya yasiyofaa ni vema kutumia njia nzuri.
“Hata vitabu vya dini vinatuelekeza kutii mamlaka iliyopo na mamlaka yoyote imewekwa na Mungu hivyo lazima watu wanapaswa kuheshimu mamlaka,” alisema Mshama.
Aidha alisema anatoa pole kwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu kwa kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana hivi karibuni mkoani Dodoma.
“Tunampa pole Tundu Lisu kwa kujeruhiwa na tunaamini watu waliohusika na tukio hilo watakamatwa tu na wananchi ndiyo watakaojua wafanywe nini watu hao,” alisema Mshama.
Alibainisha kuwa kwa sasa nchi imeingia kwenye matukio ambayo si ya kawaida ikiwa ni pamoja na watoto kutekwa watu kujeruhiwa kwa silaha utamaduni ambao si Wawatanzania na haupswi kuungwa mkono.
“Matukio kama haya na mengine ya ukatili kama yaliyokuwa yakitokea wilaya ya Kibiti ya kuwaua watu wasio na hatia ni mambyo mabaya na serikali imedhamiria kupambana nayo kwa nguvu zote,” alisema Mshama.
Aliwataka Watanzania kuendelea kuiombea nchi imani ili iendelee kuwa Kisiwa cha amani na kuachana na watu wanaotaka kuichafua nchi ili ionekane ina matatizo.
Mwisho.
John Gagarini, Kibaha
WATUMISHI wa Umma ambao wanaotumia vyeti vya kughushi wametakiwa kujiondoa wenyewe kwani endapo watabainika watapelekwa kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na kurudisha fedha wanazojipatia kupitia mishahara.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angela Kairuki wakati akizungumza na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Mji Kibaha.
Kairuki alisema kuwa watumishi wa umma nchini wanaotumia vyeti vya kughushi au visivyo vyao wajiondoe wenyewe mara moja katika utumishi wa umma kwani wakiendelea kukaa itawagharimu na endapo watabainika watatakiwa kurejesha mishahara ya miezi yote waliyoiibia serikali.
“Hata kwa upande wa watumishi ambao hawajahakikiwa kwenye zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi nao wanatakiwa wajiondoe kwani wakibainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao na fedha wanazolipwa kupitia mshahara watazirudisha,” alisema Kairuki.
Alisema kuwa makatibu tawala wa mikoa wanapaswa kuangalia na kujiridhisha na majina ya watumishi kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma na ya kwenye zoezi la uhakiki kama yanafanana.
“Majina yalioonekana kwenye zoezi la uhakiki ndiyo yanayopaswa kuonekana kwenye orodha ya ya malipo ya mishahara na kama kuna mtumishi hajahakikiwa anatakiwa aondolewe kwenye malipo ya mshahara,” alisema Kairuki.
Aidha alisema kuwa serikali itaendelea na zoezi kuhakikiwa watumishi hadi itakapojiridhisha kuwa hakuna watumishi ambao hawana sifa kwenye utumishi wa umma.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment