Thursday, October 19, 2017

WAWILI WASHIKILIWA NA POLISI KWA KUKUTWA NA MAGUNIA SABA YA BHANGI



Na John Gagarini, Kibaha


WATU wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Pwani kwa tuhuma za kukutwa na magunia saba ya dawa za kulevya aina ya bhangi yenye uzito wa kilogramu 7,500.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Jonathan Shana alisema kuwa watuhumiwa hao waligundulika baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali.

Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea huko Kwa Mathias wilaya ya Kibaha baada ya askari waliokuwa doria kupata taarifa juu ya ajali ya gari.

“Watuhumiwa hao walikuwa kwenye gari namba T847DHT aina ya IST ambalo lilipata ajali kwenye eneo hilo na baada ya kufika walianza kuwaokoa na ndipo walipokuta na gunia saba za bhangi hiyo ikiwa kwenye hilo gari ikiwa imehifadhiwa kwenye magunia ya salfeti,” alisema Shana.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kundaeli Mbowe (24) ambaye ni dereva wa gari hilo na mkazi wa Kiwalani Jijini Dar es Salaam na Ally Mtena (28) mfanyabiashara na makazi wa Gongolamboto.

Aidha alisema kuwa watuhumiwa hao wanashikiliwa ili kuweza kuchukuliwa hatua za kisheria na kujua bhangi hiyo waliitowa wapi na walikuwa wakiipeleka wapi.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment